Sura mpya ya 'Baba' baada ya salamu
Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga amechukua sura mpya tangu Machi 9, 2018 alipoamkuana na Rais Uhuru Kenyatta. Alibadilika ghafla na sasa si tena kigogo wa upinzani aliyefahamika Afrika na duniani kote kwa ukakamavu wa kisiasa.
Tofauti na awali alipokuwa mkosoaji mkuu wa serikali, Bw Odinga ameacha kulaumu serikali, amepunguza mikutano yake na wanahabari na kueleza kauli zake katika mitandao ya kijamii.
Pia amejitenga na wanasiasa wa upinzani na washirika wake waliokuwa na misimamo mikali kama yeye. Badala yake, ratiba yake imekuwa ya kuwapokoea mabalozi, makundi ya wazee na wakosoaji wake wa zamani kama vile Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.
Kabla ya kuamkuana na Rais Kenyatta, Bw Odinga alikuwa mstari wa mbele kukashifu Serikali kwa kukopa sana kutoka nchi za kigeni kwa kile alichokuwa akionya kuwa hatua hatari kwa uchumi. Lakini majuzi Serikali ilipokopa mabilioni ya pesa za Eurobond, Bw Odinga hakusema chochote.
Amekuwa msiri hivi kwamba kufikia sasa, hakuna anayefahamu aliyokubaliana na Rais Kenyatta isipokuwa taarifa ya pamoja waliyotoa kwa Wakenya hapo Machi 9 walipotangaza mwafaka.
Jumanne, Bw Odinga aliambia mkutano wa Baraza Kuu la ODM kwamba hivi karibuni yeye na Rais Kenyatta wataandaa misururu ya mikutano kote nchini kuelezea yaliyomo kwenye mkataba wao wa maelewano (MOU).
Kiongozi huyo pia amekuwa kimya kuhusu masuala mengine ambayo hapo awali angekuwa amezungumzia.
Haya ni kama vile juhudi za Serikali kukabiliana na mafuriko ambayo yamekumba maeneo mengi ya nchi ambapo hatua za kusaidia waathiriwa zimeonekana kutotosha.
Hajasema chochote kuhusu ukosefu wa usalama eneo la Kapendo katika mpaka wa Turkana na Baringo ambapo watu watano waliuawa majuzi.
Pia hajazungumzia mauaji ya wanajeshi 8 wa KDF katika eneo la Dhobly nchini Somalia mnamo Jumatatu, licha ya msimamo wake wa awali kuwa wanajeshi hao waondolewe Somalia.
Kabla ya Machi 9, Bw Odinga pia alikuwa mwepesi wa kuitisha vikao vya wanahabari mara kwa mara katika ofisi yake ya Capitol Hill Square ambapo alikuwa akikosoa serikali.
Baada ya kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta vikao vyake na wanahabari vimepungua na mtindo wake siku hizi ni kutuma taarifa moja moja kwa vyombo vya habari kupitia kwa msemaji wake Dennis Onyango.
Jumanne, Raila aliambia wajumbe wa ODM kwamba analenga kuona Kenya mpya katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.