• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Nyoro atoa maelezo jinsi serikali yake inavyojizatiti kuboresha hali ya maisha ya wakazi

Nyoro atoa maelezo jinsi serikali yake inavyojizatiti kuboresha hali ya maisha ya wakazi

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu inazidi kujiandaa iweze kukabiliana na Covid-19 kwa kuweka vitanda katika hospitali tofauti.

Gavana wa kaunti hiyo Dkt James Nyoro alisema tayari wametenga Sh100 milioni za kukabiliana na maswala ya Covid-19 kwa mpango wa kutayarisha hospitali ili kuziweka tayari kwa mkurupuko wowote wa Covid-19.

“Hatutaki kulaza damu ili kugonjea dakika ya mwisho ili tuanze kujishughulisha bali tunataka kuwa tayari kwa jambo lolote lile,” alisema Dkt Nyoro.

Kwa kile kilichoonekana kama kumchamba mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina bila kumtaja jina alimshutumu kwa kuingilia miradi ya kaunti akidai ni maendeleo yake.

“Kila kiongozi ni sharti ashike laini yake bila kutaka kuingilia miradi isiyo yake,” alifafanua Dkt Nyoro.

Alisema hospitali ya Tigoni tayari ina vitanda 230 vya wagonjwa wa Covid-19. Nayo Wangige Level 4 ina vitanda 200.

Aliongeza kusema kuwa hospitali ya Ruiru inatarajia kupata vitanda 150 vya aina hiyo.

Alisema wazee waliolemewa na maradhi tofauti kama kisukari ama shinikizo la damu watapata usaidizi kutoka kwa serikali yake.

Alisema kwa sababu ya uzee wao unaofanya baadhi wanashindwa kutembea, watatibiwa katika hospitali zilizo karibu na makazi yao.

Alisema kutokana na wingi wa watu katika mtaa wa Makongeni, Thika, wanapanga kujenga hospitali kubwa eneo hilo.

“Mimi lengo langu kuu ni kuona ya kwamba kwa miaka miwili iliyosalia ninakamilisha miradi yote muhimu ambayo iko katika mpango wetu katika Kaunti ya Kiambu,” alisema Dkt Nyoro.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa alipozuru Thika ili kuzindua mradi wa barabara katika mtaa wa Biafra na eneo la Kilimambogo, Thika Mashariki.

Alisema baadhi ya miradi inayokaribia kukamilika ni kusambaza maji katika maeneo kavu, kukarabati barabara zote za mashinani na kufanikisha mpango wa wakazi Thika Mashariki kupokea mahindi na mbolea ili waweze kupunguza makali ya njaa katika makazi yao.

Alisema kwa wakati huu watafanya juhudi kuona ya kwamba wanasaidia Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza ajenda zake nne muhimu.

Aliandamana na naibu wake Bi Joyce Ngugi, mshauri wake wa masuala ya siasa Askofu David Gakuyo, na MCA wa Thika Mjini, Bw Andrew Kimani, ambao walikiri mbele ya wananchi kuwa wataendelea kufanya naye kazi ili kuafikia ajenda zote za Kaunti ya Kiambu.

Alisema kwa muda huo wa miaka miwili iliyosalia hana muda wa kupiga siasa bali anatamani kukamilisha miradi yote iliyo mbele yake.

You can share this post!

Aliyejifanya polisi atiwa nguvuni

Moyes pua na mdomo kuiongoza West Ham United kukwepa shoka...

adminleo