Nyoro sasa 'awachorea mipaka' wabunge kutoka Kiambu siasa zikichacha
Na LAWRENCE ONGARO
SIASA za Kaunti ya Kiambu zinaendelea kupamba moto huku viongozi wakizidi kurushiana cheche za maneno kuhusu hali ya maendeleo.
Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alimsuta mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, kuwa ni kikwazo kwa maendeleo eneo pana la Thika.
“Tumechoshwa na siasa za kila mara za kuhujumu maendeleo katika maeneo mengine. Kiongozi yeyote ni sharti atulie pahala pake pa kazi,” alisema Dkt Nyoro.
Bila kumtaja jina hadharani alisema viongozi wengine wamezoea kuingilia himaya ya wenzao bila kuweka zingatio katika maeneo yao.
Aliyasema hayo mjini Thika alipokuwa akijionea miradi ya maendeleo katika sehemu tofauti.
Alimtaka mbunge huyo atangaze msimamo wake wa kisiasa kwa kusema anashabikia chama kipi, badala ya kujificha katika uliokuwa ugombea wake wa kujitegemea yaani Independent.
Kwa upande wake mbunge wa Thika Bw Wainaina alisema shutuma kutoka kwa viongozi wenzake hazitamshtua hata kidogo kwa sababu anaelewa anakotoka na anakoelekea.
“Ninanajua kazi ninayofanyia wananchi inaeleweka na wengi na kwa hivyo visingizio havitanishtua,” alisema Bw Wainaina.
Alisema tayari amejenga vibanda zaidi ya 10 kwa wahudumu wa bodaboda eneo la Kiambu na ndiyo maana kufanya hivyo kumewasababishia tumbojoto viongozi wachache.
Naye Askofu wa kanisa la Calvary Chosen Church mjini Thika, Bw David Gakuyo Ngari alimshauri mbunge huyo atekeleze wajibu wake bila kupitia mipaka ya viongozi wengine.
“Kila kiongozi amepewa mahali pake pa kufanya kazi na kwa hivyo kuingilia kazi za wengine ni makosa,” alisema Bw Ngari.
Alisema hata yeye ni kiongozi mtarajiwa ambapo “wananchi wakinipendekeza kuwa kiongozi wao mimi ni nani nikatae?”
Aliahidi ataendelea kuwapa waumini wa kanisa chakula japo kidogo kwa sababu homa ya Covid-19 imesababisha masaibu mengi katika familia.
Alisema watakuwa na kibarua kikubwa cha kuwapa ushauri wa kiroho Wakrito watakaohudhuria kanisa kwa maombi.
Alishauri kwamba wakati huu mgumu ni vyema viongozi kuja pamoja kwa maelewano ili kutumikia wananchi ipasavyo.
“Mimi kama mshauri wa gavana nitafanya juhudi kuona ya kwamba viongozi wanakuja pamoja kwa lengo moja la kutumikia wananchi,” alifafanua askofu huyo.