• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Patrick ‘Jungle’ Wainaina amchanua Ruto namna ya kuimarisha uchumi

Patrick ‘Jungle’ Wainaina amchanua Ruto namna ya kuimarisha uchumi

NA LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Kenya Kwanza bado ina nafasi ya kuimarisha uchumi wa nchi iwapo itapanga mikakati ipasavyo.

Aliyekuwa mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amesema anaunga mkono matamshi ya Rais William Ruto kwamba ipo haja ya kuibuka na mikakati ya kuimarisha uchumi katika nyakati hizi ngumu ambapo Wakenya wengi wanalemewa na gharama ya juu ya maisha.

Hata hivyo, Bw Wainaina anasema mawaziri na makatibu katika serikali ya Kenya Kwanza wameonyesha mwelekeo tofauti kwa kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje huku “tukikosa kurekebisha mipango yetu.”

“Tunastahili kufufua baadhi ya viwanda vyetu vilivyofungwa ili ajira kwa vijana iweze kupatikana,” alisema Bw Wainaina.

Alisema ni kosa kubwa kuagiza samaki kutoka nje ilhali kuna samaki wengi katika maziwa mengi nchini.

Alisema bidhaa za juakali zinastahili kupewa nafasi zaidi ili vijana waweze kubuni kazi zao wenyewe.

“Hakuna haja ya kuagiza bidhaa kutoka China, nyingi ya bidhaa hizi zikiwa zile zinazoweza kuundwa na vijana wa sekta ya juakali,” alisema kiongozi hiyo.

Pia alitoa mfano wa uagizaji wa mafuta ya kupikia chakula yaliyoagizwa hivi majuzi ya kiwango cha tani 125,000 elfu kutoka nje.

“Mpango wa aina hiyo huvunja mipango ya kampuni zetu hapa nchini na pia husababisha kampuni hizo kufuta wafanyakazi kwa ukosefu wa soko kwa bidhaa zao,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo katika mkutano wa viongozi kutoka Mlima Kenya uliofanyika mjini Thika.

Bw Wainaina aliitaka serikali kubuni kazi kwa wingi ili vijana wengi wasio na ajira wanufaike.

Alishang’aa ni kwa nini serikali ina mpango wa kusafirisha macadamia hadi China ili yapakiwe huko baada ya kutengenezewa hapa nchini.

Alisema uchumi wa Kenya itaimarika iwapo kila mikakati itafuatiliwa ipasavyo ili kuzuia ufisadi.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a alipongeza serikali kwa kuwajali vijana kwa kuwapa ajira.

Hata hivyo, alisema wale wamepewa kazi hizo ni lazima waonyeshe mwelekeo mwema ili Kenya iwe kielelezo kwa wengine walio nyuma yao.

Alisema serikali ya Rais Ruto imejali sana vijana kwa kuwapa kazi serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuajiri walimu 20,000

AMINI USIAMINI: Fahamu kumhusu mjusi kafiri anayeitwa...

T L