Siasa

JAMVI: Ishara zajitokeza Moi ndiye mrithi wa Uhuru 2022

July 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHARLES WASONGA

MATUKIO mbalimbali katika siku chache zilizopita yameibua minong’ono katika ulingo wa siasa, kwamba huenda Rais Uhuru Kenyatta anamwandaa Seneta wa Baringo, Gideon Moi kuwa mrithi wake 2022.

Kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa Rais Kenyatta, mawaziri watatu walizuru Kaunti ya Baringo kwa shughuli mbalimbali za kikazi lakini hawakuchelea kushabikia ukuruba wa kisiasa kati ya bosi wao na Seneta Moi.

Kilichovutia hisia za wadadisi ni kwamba mawaziri hao; Peter Munya (Kilimo), Joe Mucheru (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – ICT) na Sicily Kariuki (Maji) walitembelea Baringo ndani ya wiki moja ambapo seneta huyo alimwakilisha Rais Kenyatta katika hafla ya kutawazwa kwa Rais mpya wa Malawi, Bw Lazarus Chakwera.

Wadadisi wanasema Rais Kenyatta alimtuma Bw Moi Malawi katika hatua inayoashiria kuwa amekosa imani na naibu wake, Dkt William Ruto, ambaye ndiye aliyepaswa kumwakilisha katika shughuli kama hiyo ya kidiplomasia.

Waziri wa kwanza kutua Baringo alikuwa Bw Munya ambaye alizindua shughuli ya chanjo ya mifugo katika maeneo ya Loruk (eneobunge la Tiaty) na Emining (eneobunge la Mogotio).

Munya ambaye aliandamana na masaidizi wake Lina Jebii Kilimo na Katibu wa Wizara hiyo Harry Kimtai, alitumia majukwaa hayo kuwasilisha “salamu” kutoka kwa Seneta Moi.

Alifuatwa na Bi Kariuki mnamo Juni 30 ambaye alielekea hadi eneobunge la Eldama Ravine kukagua ujenzi wa bwawa la Chemususu.

Siku mbili baadaye ilikuwa zamu yake Waziri Mucheru ambaye alifika eneo la Radat, eneobunge la Mogotio kuzindua mtandao wa 4G unaodhaminiwa na kampuni za Google Loon na Telkom Kenya.

Wakati mmoja, Bw Mucheru aliwachangamsha wakazi alipounganisha kwa njia ya simu Rais Kenyatta aliyewahutubia ambapo aliwahimiza kuuza asali yao na bidhaa nyinginezo kwa njia ya mtandao ili kuwafikia wateja wengi.

“Ninataka muuze asali ya Baringo kupitia mtandao. Ni asali bora zaidi ulimwenguni na mwaweza kupata wanunuzi wengi na hivyo mkajiimarisha kimaendeleo,” Rais Kenyatta akanukuliwa akisema.

Bw Mucheru aliwaambia wakazi kwamba Seneta Moi ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) amekuwa akimsukuma kuzindua mradi ambao unalenga kufaidi kaunti nyinginezo kama vile Elgeyo-Marakwet, Uasin Gishu, Nakuru, Kakamega, Kisumu, Kisii, Bomet, Kericho na Narok.

“Nina furaha kuwa sasa ninaweza kumpa ripoti kwamba Baringo imeunganishwa kikamilifu.”

“Ninajua kuwa pahala alipo sasa amefurahi kuwa tumeweza kutimiza baadhi ya ahadi tulizotoa kwamba hatimaye tutaunganisha nchi yote kwenye mtandao wa 4G,” Waziri Mucheru akaongeza.

Haya yalijiri siku chache baada ya kukamilika kwa mchakato mzima wa kuwakomoa kabisa wandani wa Dkt Ruto kutoka uongozi wa Seneti na Bunge la Kitaifa na kuteuliwa kwa wajumbe wa Kanu katika nafasi za hadhi ya juu katika mabunge hayo mawili. Hatua hiyo ilijiri siku chache baada ya Kanu kutia saini mkataba wa muungano na Jubilee, hivyo kukifanya chama hicho cha jogoo kuwa na idhini kamili ya kuendesha ajenda za maendeleo za serikali.

Mbali na Seneta wa Pokot, Bw Samuel Poghisio aliyetunukiwa wadhifa wa Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket, ameteuliwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Sheria za Ziada (Delegated Legislation). Kamati hii zamani iliongozwa na Mwakilishi Mwanamke wa Uasin Gishu, Bi Glady Shollei ambaye ni mshirika wa Dkt Ruto.

Kamati ya Sheria za Ziada pamoja na Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na Kamati ya Bajeti ambazo zinaongozwa na wandani wa Rais Kenyatta, Mbunge wa Kangema, Bw Muturi Kigano na mwenzake wa Kieni, Bw Kanini Kega, mtawalia, zitakazoendesha mchakato wa utekelezaji wa ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) na mageuzi ya katiba kupitia kura ya maamuzi.

Mbunge wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo na mwenzake wa Kandara, Bi Alice Wahome, ambao ni wafuasi sugu wa Naibu Rais walipokonywa uongozi wa JLAC sawa na mwenzao, Bw Kimani Ichung’wa aliyefurushwa kutoka Kamati ya Bajeti.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Vincent Kimosop anafasiri matukio hayo kama sehemu ya mkakati mpana wa kumjenga Seneta Moi na kumweka katika nafasi bora katika siasa za urithi wa Rais Kenyatta.

“Bila shaka haya si matukio ya kisadfa. Ajenda kuu ya Rais Kenyatta ni kunyofoa ushawishi wa naibu wake katika ngome yake ya Rift Valley,” anasema.

Bw Kimosop anaongeza, “Kwa sababu wema huanzia nyumbani, bila shaka Rais Kenyatta anamwandaa Gideon. Swali ni je, mbona kiongozi wa hadhi ya Seneta kumwakilisha Rais nchini Malawi ilhali Naibu Rais Dkt Ruto alikuwepo nchini?”

Si siri kwamba Seneta Moi ameanza mikakati kabambe ya kujinadi katika eneo la Rift Valley na ngazi ya kitaifa kwa ushirikiano na nyota wengine wa kisiasa kutoka eneo hilo kama vile Gavana wa zamani wa Bomet, Bw Isaac Ruto.

Majuzi Bw Moi aliunda Kamati maalum itakayoongoza harakati za kuvumisha Kanu katika pembe zote za nchi, kwa kufufua matawi yake yote.

Miongoni mwa wanachama wa kamati hiyo itakayooongozwa na Seneta Poghisio ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Kenya (COTU) Francis Atwoli.

Mbali na hayo, wiki jana Kanu ilizindua rasmi mpango wa kusajili wanachama wapya, shughuli ambayo Katibu Mkuu, Bw Nick Salat anasema ni sehemu ya maandalizi yao kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mtaona mabadiliko makubwa ndani ya Kanu kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2022. Tumeanza kusajili wanachama wapya na kufufua matawi yetu kote nchini. Na muhimu zaidi ni kwamba sisi ni washirika wakuu serikalini na nia yetu ni kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Rais Kenyatta kabla ya kumpisha Gideon achukue hatamu za uongozi,” akasema Bw Salat ambaye aliandamana na Seneta Moi katika ziara ya Malawi.

Na wiki jana, Mbunge wa Rongai, Bw Raymond Moi ambaye ni kaka yake mkubwa Seneta Moi “alitoboa siri” alipowaambia washindani wake waombe zaidi ili aweze kurithi kiti cha useneta wa Baringo. Kauli hiyo iliashiria kuwa Gideon hatatetea kiti hicho kwani atawania urais 2022.

Lakini kulingana na mdadisi wa siasa, Prof Herman Manyora, Seneta Moi atakuwa na kibarua kigumu kuyeyusha umaarufu wa Dkt Ruto katika ukanda wa Bonde la Ufa.

“Mizizi ya kisiasa ya Dkt Ruto imepenya zaidi katika eneo hilo kiasi kwamba Gideon atahitaji miaka mitano zaidi kuing’oa. Kwa hivyo, ushauri wangu kwake wakati huu ni kwamba atumie rungu ya marehemu babaye kujikuza kwanza kwa miaka mitano kabla ya kujitosa kwaenyeurais 2027,” anasema mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi.