• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
JAMVI: Kalonzo alivyomwokoa Ngilu kutoka kinywa cha mamba

JAMVI: Kalonzo alivyomwokoa Ngilu kutoka kinywa cha mamba

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ‘alicheza nyuma ya pazia’ kumuokoa Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu asitumuliwe ofisini na madiwani wa kaunti hiyo.

Duru zinasema kwamba ni makamu huyo wa rais wa zamani aliyemshawishi mwandalizi wa mswada huo, Bw Peter Mwikya Kilonzo kuuondoa baada ya kubainika kuwa madiwani wa Wiper hawangeweza kuupitisha.

Inasemekana kuwa viongozi wakuu wa chama cha Wiper walikuwa wamegawanyika kuhusu mswada huo huku baadhi wakimshauri Bw Musyoka kwamba haungeidhinishwa na seneti.

Miongoni mwa waliopinga mswada huo ni naibu mwenyekiti wa Wiper, Bw Mutula Kilonzo Junior ambaye alionya kuwa kutimua gavana hakufai kuwa mazoea ya madiwani.

Duru zinasema kwamba Bw Musyoka alijipata katika hali tete ikizingatiwa kuwa baadhi ya wabunge wandani wake kutoka Kaunti ya Kitui walikuwa wakiunga mswada huo wa kumtimua Bi Ngilu.

“Huku viongozi wa kitaifa wa chama wakitaka awaagize madiwani wasimtimue Ngilu, wandani wake kutoka Kaunti ya Kitui, akiwemo Seneta wa kaunti hiyo, Bw Enock Wambua walitaka ‘awabariki’ madiwani wamtimue. Hii ilimweka katika hali tete sana na ikabidi acheze nyuma ya pazia,” alisema afisa mmoja wa Wiper ambaye aliomba tusitaje jina. K

ulingana na afisa huyo, Bw Musyoka hakutaka kuonekana kuingilia majukumu ya madiwani.“Watu hawataki kusema ukweli lakini ni Bw Musyoka ndiye aliyemweleza Bw Mwikya kuondoa mswada huo kwa sasa ili kutoa nafasi ya mazungumzo.

Bw Musyoka alihisi kwamba mswada huo ungevuruga na kulemaza huduma kwa wakazi wa Kitui na kama mwanadiplomasia wa kutajika akachukua hatua bila kutangaza hadharani kwa sababu hakutaka kuonekana kuingilia masuala ya bunge la kaunti,” alisema.

Inasemekana usiku wa tarehe 14, 2020, siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa mswada wa kung’atua Bi Ngilu, Bw Musyoka alimpigia simu Bw Mwikya na kumtaka kuuondoa. Wadadisi wanasema huenda Bw Musyoka aligundua kuwa mswada huo haungefaulu au alitumia ushawishi wake kama kiongozi wa chama kuusitisha.

“Kwa vyovyote vile, kuondolewa kwa mswada huo kulitokana na mkono wa Bw Musyoka,” alisema mdadisi wa siasa za Ukambani Geff Kamwanah.

Anakiri kwamba kilikuwa kibarua kigumu kwa madiwani wa Wiper kupitisha mswada huo ikizingatiwa kuwa Bi Ngilu alikuwa amejipanga pia.

Akiondoa mswada huo, Bw Mwikya ambaye ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Kitui alisema baadhi ya madiwani waliokuwa wakimuunga mkono walikuwa wametoweka.

Siku ya kujadiliwa kwa mswada huo, zaidi ya madiwani 10 wanasemekana kupotea ghafla wakisemekana kupelekwa likizo katika mbuga la Wanyama la Tsavo, kwa nia ya kuhujumu mswada huo.

Wadadisi wanasema sababu za Bw Mwikya kwamba hawangeweza kujadili mswada huo kabla ya kwanza kujua mahali walipo madiwani waliopotea hazikuwa na msingi, kwani ungeendelea tu bila uwepo wa madiwani hao kumi.

“Madai ya mwandalizi wa mswada huo yalikuwa ni kisingizio tu. Ukweli ni kuwa alitakiwa kuuondoa au alibaini alikuwa ameshindwa maarifa na Bi Ngilu,” alisema Bw Kamwanah.

Duru zinasema kwamba licha ya kushinikizwa na wandani wake kaunti ya Kitui kuunga mswada huo, Bw Musyoka alihisi kwamba haikuwa njia bora ya kutatua masuala ya kaunti yake ya nyumbani.

“Kwanza, hakuchochea mswada huo ilivyodaiwa na Bi Ngilu na wandani wake. Pili, kutimuliwa kwa Bi Ngilu kungewapatia wapinzani wake wa kisiasa eneo la Ukambani nguvu za kumpiga vita.

Baada ya kupima kila hali, hakuwa na budi kuhakikisha mswada huo haukujadiliwa,” alisema mdadisi wa siasa Peter Syanga.

Aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama na gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na mwenzake wa Machakos Alfred Mutua wameungana kukosoa Bw Musyoka.

Duru nyingine zilisema kwamba Bw Musyoka alihisi kuwa haukuwa wakati mzuri wa vita vya kisiasa wakati huu wa janga la corona.

Kulingana na Bw Kamwanah, Bw Musyoka anafaa kupatanisha Bi Ngilu na madiwani, iwapo kwa kweli hakuhusika na mswada huo.

You can share this post!

Simu ya video ya Rais yachangamsha kijiji

Kaunti yaambiwa ianze kufunga vituo vya corona

adminleo