Habari Mseto

Kaunti yaambiwa ianze kufunga vituo vya corona

July 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuhamisha vituo vyote vya wagonjwa wa Covid-19 vilivyo katika taasisi za elimu huku wizara ya elimu ikijitayarisha kwa ufunguzi wa vyuo vikuu na vile vya mafunzo ya anuai.

Serikali ya kaunti ya Mombasa imejipata njia panda kwenye vita vyao dhidi ya virusi hivyo baada ya kutakiwa kuhama kwenye chuo kikuu cha Mombasa na ile ya Kenya National Coast Polytechnic ambapo wagonjwa wenye akili taahira wanaopambana na virusi hivyo wanatibiwa.

Chuo Kikuu cha Mombasa ndicho kituo kikubwa zaidi cha wagonjwa wa corona chenye vitanda 300.

Hivi majuzi waziri wa afya Bw Mutahi Kagwe aliipongeza serikali ya Mombasa kwa kuwa na kituo cha kipekee nchini cha kuwapa huduma za afya wagonjwa wenye akili taahira wanaokabiliana na janga la corona.

Lakini huku serikali ikijitayarisha kwa ufunguzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu, serikali ya Gavana Joho itatakiwa kutafuta suluhu ya sehemu itawapeleka wagonjwa wa corona.

Kamishna wa Mombasa ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya kukabiliana na janga hilo kaunti hiyo Bw Gilbert Kitiyo aliwahakikishia wanafunzi wa vyuo hivyo na wahadhiri kwamba sehemu zilizotumika kama vituo vya kuhifadhi wagonjwa vitanyunyuziwa dawa maalum. ili kuhakikisha usalama wao.

‘Tumewaandikia barua serikali ya kaunti ya Mombasa kuhamisha kituo chao kilichoko pale chuo kikuu na kile cha ufundi ili tuanze matayarisho ya ufunguzi wa vuo hivyo mnamo Septemba. Hata hivyo tutanyunyuzia sehemu hizo dawa, kufanya marekebisho kabambe kabla ya kufungua. Tutachukua tahadhari zote,’ alisema Bw Kitiyo.

Aprili mwaka huu gavana wa Mombasa Hassan Joho alizindua rasmi kituo hicho cha kuwatibu wagonjwa ambao si mahututi.

Hata hivyo kwenye mahojiano na kituo cha radio hivi majuzi, afisa wa afya Dkt Khadija Shikely alisema serikali ya kaunti imeanza kuweka mikakati ya kutafuta sehemu mbadala ya kuwahamisha kituo hicho.

“Tunaanza kuweka mikakati ya kutafuta sehemu mbadala lakini tunaona hospitali ya Port Reitz ikiwa mwafaka,” alisema Dkt Shikely.