Viegesho vya kwanza vya mizigo bandari ya Lamu vyakamilika
MRADI mkubwa Pwani wa kujenga Bandari ya Lamu (LAPSSET) umepiga hatua baada ya ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza vya mizigo kukamilika.Ujenzi huo uliogharimu serikali ya kitaifra kima cha Sh48 bilioni ulianza mwaka 2016.
Akithibitisha kukamilika kwa viegesho hivyo jana, Afisa Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi na Maendeleo ya Lapsset (LCDA), Bw Silvester Kasuku, alisema ujenzi wa viegesho hivyo ulikamilika mwezi huu.Gati zote tatu zina urefu wa kilomita 1.2 ilhali upana wake ni karibu mita 18.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Kasuku alisema bodi yake kwa sasa imebaki na kazi ya kuandaa hafla ya kuzindua rasmi viegesho hivyo.
Hatua hiyo itaashiria uzinduzi wa biashara katika bandari hiyo mpya, ambao unaaminika kwamba utachangia ustawishaji uchumi Kenya hasa kiviwanda.Bandari hiyo pia inategemewa kusafirisha mafuta kutoka Kenya hadi mataifa ya nje wakati uzalishaji rasmi utakapoanzishwa Turkana.
Bw Kasuku aidha alisema huenda shughuli ya kuzindua gati hizo ikacheleweshwa kufuatia maradhi yanayoendelea nchini na ulimwengu mzima ya Covid-19.
“Itabidi tusubiri kwa muda usiojulikana kabla ya gati hizo kuzinduliwa. Haya yote ni kutokana na virusi vya corona ambavyo bado vinahangaisha nchi na ulimwengu,” akasema Bw Kasuku.
Bandari ya Lamu imepangwa kuwa na jumla ya gati 32.Meneja wa Lapsset, tawi la Lamu, Salim Bunu, alimsifu mwanakandarasi wa ujenzi wa Lapsset kwa kuendeleza shughuli zake za ujenzi wa mradi huo licha ya kuwepo kwa changamtoto za Covid-19.
Bandari ya Lamu inajengwa na Kampuni ya Ujenzi kutoka nchini China (CCCC).Alisema anaamini kukamilika kwa mradi wa Lapsset kutaimarisha zaidi biashara na miundomsingi kwenye kaunti nzima ya Lamu.
“Eneo hili zamani lilikuwa likmesahaulika kimiundomsingi na maendeleo mengine, ikiwemo barabara.
Tunashukuru kwamba ujio wa Lapsset umekuwa mibaraka kwetu kwani barabara zinajengwa. Tunatarajia viwanda kujengwa eneo hili hasa punde bandari ya Lamu itakapoanza kutekeleza shughuli zake,” akasema Bw Bunu.