HabariSiasa

Handisheki yageuza 'Baba' bubu

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA WAANDISHI WETU

KIMYA kirefu cha Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusiana na hatua za serikali zinazoenda kinyume na misimamo yake ya zamani, kimemsawiri kama kiongozi aliyebanwa kisiasa.

Kwa muda mrefu, Bw Odinga amejitokeza kama mtetezi wa demokrasia, mpiganiaji wa haki na usawa kimaendeleo na mtetezi wa haki za walalahoi.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa upinzani amefyata ulimi tangu akumbatiane kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018 licha ya matukio yanayoendelea kukera wananchi kama vile ubomoaji wa nyumba na masoko kiholela, udhalimu wa polisi dhidi ya raia, na pendekezo jipya kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti.

Mfumo mpya wa ugavi wa fedha uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA) utahitaji fedha zigawanywe kwa msingi wa idadi ya watu katika kaunti badala ya ukubwa wa kaunti.

Umepingwa na viongozi, hasa wa Pwani na Kaskazini, ambao wanalalamika utachangia maeneo yao kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo.

Ilibainika kuwa, Rais Uhuru Kenyatta anataka Seneti ipitishe hoja ya kuruhusu mfumo huo mpya haraka ili kuzuia mtafaruku wa kisheria.

Wadadisi wanasema Bw Odinga yumo kwenye njiapanda kwa kuwai, kwa upande mmoja, yeye ni mtetezi sugu wa haki kwa wananchi lakini kwa upande mwingine, hangependa kumuudhi Rais Kenyatta.

“Matumaini ya Bw Odinga kushinda urais 2022 iwapo ataamua kuwania yamo mikononi mwa Rais Kenyatta. Iwapo ataanza kukosoa serikali, kutakuwa na hatari ya wawili hao kutofautiana kabla ya 2022,” asema mchanganuzi wa siasa, Prof Medo Misama.

Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupinga mfumo huo kwa niaba ya viongozi wa Pwani, alisema amechukizwa na jinsi ODM inavyotaka kuchangia katika hatua ambayo itaumiza eneo lililo na wafuasi wake wengi.

“Tuna haki ya kujua ni nini kilitokea na ni lazima ukweli usemwe. Itakuaje Kilifi ipoteze Sh1.2 bilioni na maeneo mengine kama Mandera pia kupoteza hadi Sh2 bilioni ilhali ni maeneo yasiyo na hospitali, barabara wala shule za kitaifa?” akasema.

Aliyekuwa Mbunge wa Garsen, Bw Danson Mungatana aliomba maseneta kujitenga na uaminifu wao kwa vigogo wa kisiasa akiwemo Bw Raila watakapofanya uamuzi.

“Haya ndiyo mambo ambayo hufanya watu waanze kudhukia nchi zao na kuwazia kujitenga,” akasema.

Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, alisihi maseneta wasipitishe hoja itakayoruhusu utekelezaji wa mfumo huo.

Alisema walioupendekeza hawakutilia maanani kwamba, wakati mfumo wa ugatuzi ulianzishwa, kuna kaunti zilikuwa zimenufaika sana kimaendeleo kuliko kaunti nyingine.

“Itatubidi tufutilie mbali mipango yote ya maendeleo kwa sababu fedha zitakazobaki zitakuwa ni za mishahara pekee,” akaeleza.

Mbunge wa Kacheliba, Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Mark Lomunokol, alisema kupitishwa kwa mfumo huo kutadhihirisha viongozi wanahadaa Wakenya wanaposema wanataka kuleta umoja na haki kitaifa.

Gavana wa Bungoma, Bw Wycliffe Wangamati ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Baraza la Magavana alisema, kaunti yake ni mojawapo ya tano ambazo zina watu takriban milioni 1.8.

“Bungoma ni kaunti ya tano kwa wingi wa watu baada ya Nairobi, Kakamega, Nakuru na Kiambu. Naunga mkono mfumo huo mpya wa kugawa fedha lakini naomba kaunti zilizoachwa nyuma pia zitafutiwe jinsi zitalindwa,” akasema.

Bw Odinga, katika mahojiano na kituo kimoja cha redio miezi miwili iliyopita alisema hajazuia viongozi wa ODM kukosoa serikali ya Rais Kenyatta inapofanya mambo isivyostahili.

“Serikali ikienda kombo, wabunge ambao ni wawakilishi wa watu wako huru kuishutumu. Wakitaka kumfikia Rais Kenyatta wanaweza kupitia kwangu niwasaidie kumfikia,” alisema Bw Odinga.

Lakini baadhi ya wabunge kutoka Nyanza waliambia Taifa Leo imekuwa vigumu kwao kukosoa serikali hadharani kutokana na hofu ya kutengwa na kuhatarisha kushindwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Ripoti za Leonard Onyango, Brian Ojamaa, Charles Lwanga, Stephen Oduor, Oscar Kakai na Valentine Obara