Ngirici apinga kung'olewa kitini Kewopa
Na SAM KIPLAGAT
MWAKILISHI wa Wanawake Kaunti ya Kirinyaga, Bi Purity Ngirici ameenda mahakamani kupinga kuondolewa kwake kutoka wadhifa wa Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge Wanawake (Kewopa).
Mbunge huyo ni miongoni mwa viongozi walio wandani wa Naibu Rais William Ruto ambao wameendelea kupokonywa vyeo vyao bungeni kwa wiki kadhaa sasa.
Bi Ngirici anasema kuwa kikao kilichoandaliwa Julai 7, ambacho kilitumiwa kupitisha uamuzi wa kumwondoa kilikuwa haramu.
Kulingana naye, kikao hicho hakikuwa na idadi ya wanachama wanaotakiwa ili kupitisha maamuzi muhimu ya chama.
Mwakilishi wa Kike wa Kiambu, Bi Gathoni Wamuchomba ndiye aliteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Kewopa.
Mbunge huyo ameshtaki Mwakilishi wa Kike wa Kiambu Bi Wamuchomba, Rosa Buyu (Kisumu) na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko.
Jaji James Makau aliorodhesha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuwataka walioshtakiwa kuwasilisha majibu yao kuhusu malalamishi ndani ya siku mbili.
Kesi hiyo itatajwa tena Julai 23, mwaka huu, ili korti iweze kuthibitisha ikiwa maagizo yaliyotolewa na mahakama yatakuwa yamezingatiwa.
Kulingana na Bi Ngirici, viongozi wa Kewopa huchaguliwa mwanzoni mwa muhula wa miaka mitano na wanatakiwa kuhudumu hadi bunge litakapovunjiliwa mbali kupisha uchaguzi mkuu unaofuatia.
Anasema kuwa hatua ya wanachama kumwondoa kabla ya Bunge kuvunjwa inakiuka Kifungu cha 6(b) cha Katiba ya Kewopa.
Anadai kuwa wanachama walimwondoa bila kufuata utaratibu wa katiba ya muungano huo.
Bi Ngirici alisema amekuwa akidudumia chama hicho kwa uaminifu na kujitolea. Anasema wanahitajika wanachama 73 kati ya 97 ili kumwondoa mwenyekiti.
Aliongeza kuwa, muungano huo unafadhiliwa na wachama pamoja na mashirika ya kimataifa ambayo yanataka kuhakikisha kuwa kuna uwazi, demokrasia na uadilifu.
Anataka mahakama iamue kwamba Bi Wamuchomba azuiliwe kuchukua wadhifa huo hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.