• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
Uhuru apigwa breki na mahakama kuhusu mawakili

Uhuru apigwa breki na mahakama kuhusu mawakili

Na RICHARD MUNGUTI

AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta kuwa mawakili wa kibinafsi walioteuliwa kutetea idara na wizara za serikali wapokonywe kazi hizo, lilipigwa breki na Mahakama Kuu Jumanne.

Akisitisha kutekelezwa kwa agizo hilo, Jaji John Mativo alisema ushauri mwafaka haukutolewa kabla ya amri hiyo kutangazwa.

Jaji Mativo aliagiza kuwa mawakili wa kibinafsi walioteuliwa kuwakilisha serikali waendelee na kazi zao hadi kesi hiyo iliyowasilishwa na Chama cha Mawakili Kenya (LSK) itakaposikizwa na kuamuliwa.

Jaji aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuagiza itajwe mnamo Oktoba 6, 2020 kupitia kwa video.

LSK itatakuwa kuwasilisha ushahidi kwamba agizo hilo la Rais linakinzana na sheria na linakiuka haki zao.

“Nimechambua kwa makini mawasilisho ya LSK na kufikia uamuzi kwamba, kesi hii iko na mashiko kisheria na kamwe haipaswi kutupiliwa mbali,” alisema Jaji Mativo.

Baadhi ya mawaziri, akiwemo Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i na mwenzake wa Elimu, Prof George Magoha walikuwa tayari wamearifu wakuu wa idara zilizo chini yao kuanza kutekeleza agizo la Rais mara moja.

Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua pia alikuwa ameagiza kwamba mawakili wa kibinafsi wapokonywe mara moja kesi hizo.Uamuzi huo ulikuwa umefanywa Rais alipokutana na mawaziri, manaibu wao na makatibu wa wizara hivi majuzi.

Mawaziri walitakiwa kutekeleza agizo hilo katika muda wa siku 21.Pia, walitakiwa wasiteue mawakili wa kibinafsi kutetea wizara zao ama mashirika ya serikali bila idhini ya Mwanasheria Mkuu (AG).

“Mawaziri wote waagizwa kuwapokonya mawakili wa kibinafsi kesi wanazotetea serikali katika siku 21 ambazo hawakuteuliwa na AG,” alisema Bw Kinyua.

Katika maagizo hayo ya Rais, iliamuliwa pia mashirika ya serikali yaondoe kesi dhidi ya mashirika mengine ya serikali.Ingawa haikujulikana mara moja sababu ya kutolewa kwa maagizo hayo, mawakili walidai ni dhuluma dhidi ya kazi zao na watakumbwa na hasara kwa njia isiyo ya haki.

You can share this post!

Wagonjwa wa corona wanaojitokeza wasifiwa

Wiper yavunja mkataba na Nasa, yaingia Jubilee rasmi

adminleo