Matumaini ya mavuno licha ya janga la corona
Na CHARLES LWANGA
MSIMU wa mvua ulioanza Machi mwaka huu, siku chache baada ya janga la corona kubisha hodi nchini, umeletea wakulima wengi Kilifi matumaini ya mavuno bora kabla ya msimu ujao wa mvua kuanza Oktoba.
Kila mwaka, takriban watu 200,000 eneo la Malindi, Magarini, Ganze na Kaloleni huwa hatarini kuangamizwa na baa la njaa kutokana na ukame na mafuriko ambayo huharibu mimea, baada ya Mto Sabaki kuvunja kingo zake.
Bw Alex Mwangemi, mkulima wa Magarini ambaye amepanda mahindi kwenye shamba la ekari katika kijiji cha Marikebuni alisema, wanatarajia visa vya mlipuko wa njaa eneo hilo vitapungua au hata kukosekana mwaka huu.
“Kwa wale ambao walifanya ukulima kwa makini msimu huu watavuna kwa mshindo chakula ambacho kitawatosha kwa misimu miwili au mitatu ijayo,” alisema Bw Mwangemi ambaye alikuwa mfanyikazi wa hoteli zamani.
Bw Mwangemi alisema amefanya kilimo kwa miaka 30 lakini hawajawahi kupokea mvua kama ile ambayo wameshuhudia msimu huu.Vile vile, imebainika wengi walirudi kulima mashamba yao eneo hilo wakati janga la corona liliposambaratisha shughuli nyingi za kujipatia riziki.
“Kila mwaka, Magarini huwa miongoni mwa maeneo nchini ambapo inasemakana watu wanaangamia kwa njaa, lakini kile Wakenya hawajui ni kuwa eneo hili ni kati ya maeneo machache Kilifi ambayo yana mchanga wenye rotuba,” alisema.
Mkulima mwingine, Bi Rehema Benjami Thoya alisema wanatarajia mapato bora kwa sababu mvua ilikuja wakati unaofaa msimu huu na ikanyesha ya kutosha.
“Kuchelewa kupanda huwa ndio chanzo cha njaa kwa sababu tangu jadi, tumekuwa tukipanda Mei lakini msimu huu tumepanda Machi,” alisema.
Bi Thoya pia aliisifu serikali ya kaunti ya Kilifi kwa kuanzisha mradi wa kilimo uliofanya wagawiwe mbegu na mbolea za bure wakapata nafasi ya kukodisha matrekta za kulima kutoka kwa serikali kwa bei nafuu.