• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 7:55 AM
ONGAJI: Wakenya wajihadhari na wageni wanaoiba ubunifu wao

ONGAJI: Wakenya wajihadhari na wageni wanaoiba ubunifu wao

Na PAULINE ONGAJI

Kenya imetambulika kote duniani kama mojawapo ya mataifa yaliyo mstari wa mbele katika uvumbuzi hasa Afrika.

Ni uvumbuzi huu ulioleta huduma muhimu kama vile M-Pesa na ushahidi, na hivyo kulizolea taifa hili duniani kote.Hata hivyo, huku Kenya ikiendelea kupaa katika nyanja hii, kumekuwa na wasi wasi wa wizi wa mali ya wavumbuzi.

Mara kwa mara, tumesikia taarifa kuhusu kazi za wavumbuzi Afrika kuibiwa na mashirika ya kigeni.Kumekuwa na visa vya wavumbuzi barani kulalamika kuhusu raia wa nje wanavyokuja na kuiba maarifa yao, kuunda bidhaa upesi na kuzisajili kama kazi zao halisi.

Kumekuwa na tetesi za mashirika makubwa ya kigeni kuwasili kama wafadhili, na mwishowe kuwalaghai wavumbuzi ambao baadaye hutupwa nje kazi zao zinapoimarishwa na kusajiliwa na watu wengine.

Lakini hata tunapolalamika kuhusu wizi huu, sisi kama Wakenya na Waafrika kwa jumla, hatuwezi kujiondolea lawama kwa kuchangia pakubwa tatizo hili.

Kwanza, kuna mapengo katika sheria za kuwalinda wavumbuzi, suala ambalo limefanya iwe vigumu kwa wavumbuzi halisi kusajili kazi zao na kuzilinda.

Hii imefanya iwe rahisi kwa kazi zao kuibiwa hata na Waafrika wenzao, pindi wanapozianika wazi.Aidha, sheria hizi dhaifu zimefanya iwe vigumu kwa wavumbuzi wa aina hii kupata haki kazi zao zinaponakiliwa na matapeli na kusajiliwa.

Kutokana na tatizo hili, wavumbuzi wengi wanakimbilia mtandaoni kuonyesha uwezo wao pindi wanapovumbua kitu, wakidhani jukwaa hili litawapa fursa ya kuonekana.

Lakini, kwa bahati mbaya, mtandao umekuwa mtego wa wezi wanaovizia kazi halisi za wavumbuzi, kabla ya kukimbia na kuiba maarifa yao na kutoa bidhaa sawa na hizo.

Hii inanikumbusha hadithi ya bwana fulani aliyevumbua jiko spesheli linalotumia mawe maalumu, ambayo huchukua miaka kabla ya kuisha.

Licha ya uvumbuzi huu ambao bila shaka ungetoa suluhisho kwa tatizo la ukataji miti, bwana huyu alisimulia jinsi alivyotatizika katika jitihada zake za kutaka usaidizi kutoka kwa mashirika husika ili bidhaa hii iimarishwe na kusajiliwa.

Ni suala ambalo limeendelea kuathiri Afrika kiasi kwamba bara hili limesalia nyuma katika masuala ya uvumbuzi hasa wa kiteknolojia, ikilinganishwa na nchi kama Japan inayosifika kwa kuunda magari, pikipiki na kamera, au Korea Kusini ambayo ustadi wa kuunda simu na bidhaa za kieletroniki unajulikana duniani kote.

Serikali za Afrika haziko tayari kulinda maarifa ya wavumbuzi wake na walaghai wa kigeni wametambua hilo.

You can share this post!

WANDERI: Ukakamavu wa Omido ni fahari kuu kwa Maathai

ODM yajiandaa kupinga refarenda kufanywa 2022

adminleo