• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Serikali yasema mawaziri hawajazimwa kuzuru mashinani

Serikali yasema mawaziri hawajazimwa kuzuru mashinani

SAMMY WAWERU Na CHARLES WASONGA

WAZIRI Msaidizi wa Afya Rashid Aman amepuuzilia mbali ripoti kwamba mawaziri wamezimwa kuzuru maeneo mbalimbali nchini ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Akiongea na wanahabari Jumatano, jijini Nairobi Dkt Aman alisema huduma za serikali ni muhimu na haziwezi kusitishwa kabisa “hata kwa dakika moja.”

“Hata bila vikwazo kuwekwa mawaziri hawana uhuru wa kukiuka masharti ya Wizara ya Afya ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Ni sharti mawaziri wawe kielelezo cha kuigwa katika vita dhidi ya Covid-19,” Dkt Aman akasema alipokuwa ajibu maswali kutoka kwa wanahabari baada ya kutoa taarifa kuhusu hali ya janga hilo nchini.

Mnamo Jumatano, Julai 22, 2020, gazeti moja la humu nchini liliripoti kwamba Rais Uhuru Kenyatta amewaamuru mawaziri kukomesha ziara sehemu mbalimbali nchini baada ya watatu kati yao kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Duru zilisema kuwa amri hiyo ilitolewa kwa sababu mawaziri husafiri pamoja na makatibu wa wizara zao na maafisa wengine wa ngazi za juu.

Ziara hizo pia huvutia umati mkubwa wa watu na hivyo kuwaweka raia katika hatari ya kusambaza au kuambukizwa virusi vya corona.

Baadhi ya mawaziri walioathiriwa na marufuku hiyo ya usafiri ni Fred Matiang’I (Masuala ya Ndani), Joe Mucheru (ICT), Mutahi Kagwe (Afya), Ukur Yatani (Fedha) na Adan Mohammed (Utangamano wa Afrika Mashariki).

Walikuwa wameratibiwa kuzuru, Isiolo, Moyale na Marsabit kuanzia Jumatano hadi Ijumaa, lakini ziara hizo zimesimamishwa kwa muda.

You can share this post!

Wengine 637 wapatikana na corona, 10 wafariki

Wanaoteremsha maski kwa kidevu washtakiwe, asema gavana

adminleo