• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
WASONGA: Sheria itekelezwe bila kujali hadhi au tabaka

WASONGA: Sheria itekelezwe bila kujali hadhi au tabaka

Na CHARLES WASONGA

KATIBA pamoja na sheria mbalimbali zinapasa kuzingatiwa na Wakenya wote pasina kujali hadhi au mamlaka katika jamii.

Rais Uhuru Kenyatta ameshadidia, mara si moja kwamba, Kenya ni taifa linalozingatia utawala wa sheria na kwamba, hakuna anayepasa kusazwa akivunja sheria.

Lakini inaudhi kwamba katika siku za hivi karibuni, serikali imekuwa ikitekeleza sheria kwa njia inayopendelea tabaka la matajiri na kuumiza masikini.

Taswira inayojitokeza ni ile ya taifa lenye sheria mbili; moja ya masikini na nyingine ya mabwanyenye wenye ushawishi serikalini.Mifano ni mingi lakini ningependa kujikita katika mchakato wa serikali wa kukomboa ardhi ya umma na maeneo ya misitu ya serikali.

Masikini wanafurushwa kikatili, mali yao ikiteketezwa, huku wakiwekwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona ilhali mabwanyenye wanasazwa.

Hivi sasa ninapoandika maoni haya, maelfu ya wakazi wa Marioshoni, Elburgon, kaunti ya Nakuru hawana makao baada ya nyumba zao kubomolewa, na kuteketezwa, na maafisa wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu (KFS).

Sababu ni kuwa, watu hawa, wengi wao kutoka jamii ndogo ya Ogiek, wamekuwa wakiishi katika msitu wa Mau kinyume cha sheria.

Kinaya ni kwamba, hivi majuzi, serikali hii hii, ilisema iko tayari kusitisha ubomoaji wa nyumba za kifahari zilizojengwa katika ardhi iliyonyakuliwa kutoka msitu wa Ng’ong katika eneo bunge la Lang’ata.

Waziri wa Mazingira Kerioko Tobiko aliwaambia wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi, Mazingira na Mali Asili kwamba, maafisa wa wizara yake watakutana na wakazi wa mitaa ya kifahari iliyojengwa katika ardhi hiyo kwa lengo la kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo.

Swali ni, mbona ijadiliane na mabwanyenye wanaokalia ardhi ya msitu wa Ng’ong, wakidai walinunua, huku ikiwa mwepesi kuwafurusha masikini kinyama katika maeneo ya Marioshoni, Maasai Mau, Embubut, Kariobangi na Ruai?

Mbona serikali inaonekana kupendelea wakazi wa mitaa ya kifahari kama vile, Sun Valley, Royal Park na Lang’ata Gardens, ilhali sawa wakazi wa Marioshoni, waliuziwa ardhi na wanyakuzi ambao wengi wao bado wanashikilia nyadhifa za uongozi katika serikali ya sasa?

Kwa nini serikali ilikataa kujadilia na Wakenya wanaofurushwa Marioshoni au waliotimuliwa Kariobangi na Ruai ilhali mahakama ilitoa agizo kwamba, watu hawa wapewe makao mbadala kabla ya kufurushwa?

Mnamo 2018, Mahakama ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu iliitaka serikali ya Kenya kuwapa watu wa hawa makazi mbadala kabla ya wao kufurushwa, lakini sasa inaonekana kupuuza amri hiyo.

Na serikali ilipuuza agizo kama hilo lilitolewa Mei ya Jaji wa Mahakama Kuu, Nairobi, Joseph Okong’o kuhusiana na kesi iliyowasilishwa na wakazi wa Kariobangi.Kimsingi, serikali inapasa kusitisha mpango wa ubomoaji wa makazi ya watu, ambao kwa kutofahamu, walinunua ardhi ya misitu au ile iliyotengewa miradi ya serikali.

Kwa kuendelea na shughuli hiyo wakati huu wa janga la Covid-19, serikali inawaweka waathiriwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Zoezi hilo, ambalo pia linaendeshwa katika msitu wa Embobut, ambapo watu wa jamii ya Sengwer wanafurushwa, ama kwa hakika inarudisha nyuma vita dhidi ya janga hili.

Zoezi hili lapasa kuendelea baada ya Covid-19 kudhibitiwa, kwani ni muhimu.Na wale ambao walinyakua ardhi ya misitu ya Ngong’, Mau, Embubut na ardhi zingine za umma wasakwe na waadhibitiwe kwa mujibu wa sheria.

[email protected]

You can share this post!

Palace yajinasia Ferguson

WANGARI: Serikali ichukue hatua kunusuru shule za kibinafsi

adminleo