Michezo

Klabu 15 KPL zapewa Sh13m

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KLABU 15 kati ya 18 za Ligi Kuu ya soka ya humu nchini zimepokea hundi ya Sh13 milioni ambazo ni malipo ya awali kabisa kutoka kwa BetKing ambaye ni mdhamini mpya wa Ligi Kuu ya Kenya.

Kakamega Homeboyz, Nzoia Sugar na mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia hawajapokea mgao wa fedha hizo huku usimamizi wa Gor Mahia ukisisitiza haja ya kuchunguzwa mwanzo kwa mkataba kati ya FKF na BetKing ambayo ni kampuni ya mchezo wa kamari nchini Nigeria.

Klabu 17 kati ya 18 za Ligi Kuu zilihudhuria mkutano wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ambapo wenyeviti wa vikosi hivyo walikubaliana kuunda kamati maalumu ya kushughulikia uhamisho wa Ligi Kuu ya soka kutoka kampuni ya KPL.

Elly Kalekwa ambaye ni Rais wa Sofapaka, alikosa kuhudhuria mkutano huo ulioshuhudia wenyeviti Dan Shikanda (AFC Leopards), Robert Maoga (Kariobangi Sharks), Daniel Aduda (Tusker), Erick Oloo (Ulinzi Stars) na Ken Ochieng (Zoo Kericho) wakichaguliwa kuwa vinara wa kamati ya mpito itakayosimamia mchakato wa kubadilisha Ligi Kuu ya KPL hadi kuwa Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKFPL).

Kamati hiyo inatarajiwa pia kutalii uwezekano wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya kumchagua mwenyekiti huru atakayesimamia shughuli za uendeshaji wa FKFPL.

Wanakamati hao watakuwa pia na jukumu la kushauri

FKF kuhusu utaratibu wa kuboresha usimamizi wa kabumbu ya humu nchini. Wenyeviti Bob Munro (Mathare United), Cleophas Shimanyula (KK Homeboyz) na Evance Kadenge (Nzoia Sugar) walipiga kura dhidi ya wenzao watano waliochaguliwa kusimamia kamati ya mpito ya FKFPL.

Wakili Ambrose Rachier ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa KPL hakushiriki kikamilifu mkutano huo. Mbali na kutochangia hoja yoyote wakati wa mkutano, hakushiriki shughuli ya upigaji kura, kuuliza swali wala kujibu.

Mkataba wa KPL ambao wamekuwa waendeshaji wa Ligi Kuu ya soka ya Kenya, unatamatika rasmi mnamo Septemba 2020. FKF inatarajiwa kufichua mpango mwingine kuhusu udhamini wa soka ya Kenya wiki ijayo.

Kwa mujibu wa mkataba mpya wa FKF na BetKing ambayo ni kampuni ya mchezo wa kamari, klabu zitalipwa jumla ya Sh13 milioni za mwanzo siku saba baada ya makubaliano. Mwezi mmoja kabla ya kampeni za msimu mpya kuanza, klabu zitapokea Sh75 milioni kisha Sh75 milioni tena baada ya miezi mitatu.

BetKing inatazamiwa kufadhili soka ya Ligi Kuu ya Kenya kwa kima cha Sh1.2 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. FKF imethibitisha kuwa mpango huo utashuhudia kila kikosi cha Ligi Kuu ya FKFPL kikipokezwa Sh8 milioni kwa msimu.

BetKing pia imefadhili soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza kwa Sh100 milioni. Mpango huo utaendeshwa kwa miaka mitano ijayo huku kila kikosi kitakachoshiriki kivumbi hicho kikipokezwa Sh500,000 kwa mwaka.

“Hii ni mara ya kwanza katika historia ambapo soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza nchini Kenya imepata mdhamini. Ni hatua kubwa katika maendeleo ya soka yetu pamoja na makuzi ya thamani yake,” akasema Mwendwa.

Kufaulu kwa mpango huo wa udhamini kunamaanisha kwamba washiriki wote wa madaraja matatu ya soka ya Kenya wanafadhiliwa na kampuni za mchezo wa kamari. Kampuni ya Betika ndiyo inadhamini Ligi ya Kitaifa ya Daraja la Pili (NSL) huku Odibets ikifadhili ligi za soka ya mashinani.