• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Komesha ‘utikitimaji’, Kalonzo afokewa

Komesha ‘utikitimaji’, Kalonzo afokewa

NA JUSTUS OCHIENG

VYAMA vya Orange Democratic Movement (ODM), Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya, sasa vinataka chama cha Wiper kiachilie vyeo vyote kinachoshikilia katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Hii ni baada ya Wiper kuidhinisha kuhama muungano wa NASA na kuingia kwenye mkataba wa kisiasa na Jubilee.

Suala hilo huenda likazua mgongano kati ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na wenzake Musalia Mudavadi wa ANC na Raila Odinga wa ODM.

Viongozi wa ODM na ANC wanahoji kwamba kulingana na sheria za vyama vya kisiasa, Wiper haiwezi kuwa na wawakilishi bungeni ilhali imeingia kwenye makubaliano na Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alishutumu kitendo cha Wiper akisema chama chochote hakiwezi kuunga mrengo wa wengi na wachache kwa wakati mmoja.

‘Wiper ijiondoe kwenye vyeo vyote vya upande wa wachache baada ya kuungana na mrengo wa wengi. Hata hivyo, jinsi nimjuavyo kiongozi wao, huenda wana nia ya kunufaika na mrengo wa wengi na ule wa wachache kwa wakati mmoja,’ akasema Bw Sifuna.

Naibu Kiongozi wa ANC Ayub Savula na Katibu wa Ford Kenya Dkt Eseli Simiyu, pia walisema hawatakubali Wiper ikwamilie nafasi za uongozi zilizotengewa wachache ilhali imehamia mrengo wa wengi.

‘ANC na ODM zitaandika barua kwa msajili wa vyama vya kisiasa kuondoa Wiper kwenye NASA,’ akasema Bw Savula.? Mnamo Jumanne, mkutano wa Baraza Kuu la Wiper ulitoa idhini kwa Bw Musyoka kuingia kwenye mkataba na Jubilee na kuiunga mkono ndani na nje ya Bunge.

‘Kama Wiper wameondoka, basi nafasi za uongozi wanazoshikilia bungeni pia lazima waziache,’ akasema Dkt Eseli.

Watakaopoteza nafasi zao ni Kiranja wa wachache kwenye Seneti Mutula Kilonzo Jnr na Naibu Kiranja wa wachache katika Bunge la Taifa Robert Mbui.

Bw Kilonzo alikiri kwamba kisheria watapoteza nafasi zao wakirasmisha uhusiano wao na Jubilee.

Katibu wa Wiper Judith Sijeny alisema uamuzi huo uliafikiwa baada ya kubainika kwamba muungano wa NASA umekufa. Ili Muungano wa NASA uvunjwe, washirika watatu lazima wajiondoe.

Vyama wanachama ni ODM, Wiper, ANC, Ford Kenya ya Moses Wetang’ula na CCM cha aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto

You can share this post!

Viongozi wa kidini waombea Waiguru na madiwani wapatane

Inter waruka Atalanta, waikaribia Juve

adminleo