• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Wachuuzi karantini kwa kuuzia wagonjwa wa corona mayai

Wachuuzi karantini kwa kuuzia wagonjwa wa corona mayai

Na BENSON MATHEKA

WACHUUZI wawili wamewekwa karantini kwa siku 14 kwa kuingia katika kituo cha kutenga walioambukizwa virusi vya corona katika Kaunti ya Machakos kuwauzia wagonjwa mikate na mayai.

Kisa hiki kimejiri huku idadi ya watu wanaoambukizwa virusi hivyo nchini ikipanda na kufikia 17,603 baada ya visa vipya 960 kuripotiwa Jumapili ikiwa ni idadi ya kubwa zaidi kwa siku moja tangu Machi.

Kaunti ya Machakos ni miongoni mwa zilizorekodi visa vya juu vya maambukizi ya corona tangu serikali ilipolegeza masharti na kufungua kaunti za Nairobi na Mombasa.

Maafisa wa Afya wa kaunti hiyo walisema waliwasaka wawili hao kwa kuingia katika hospitali ya Kangundo kuwauzia wagonjwa wa corona mayai.

Waziri wa afya wa kaunti ya Machakos, Dkt Ancent Kituku alisema kwamba waliwapata wawili hao sokoni wakiendelea na shughuli zao.

“Tuliwapata na sasa wamewekwa karantini nyumbani lakini tumepeleka sampuli zao kupimwa katika hospitali ya Machakos Level Five ingawa hawakuwa na dalili za ugonjwa huo,” Dkt Kituku alisema.

Alisema kwamba ilithibitishwa wawili hao hawakutangamana na wagonjwa wa corona katika kituo hicho. Mnamo Jumapili, mwenyekiti wa soko la Kangundo Chris Kyalo aliripoti wakazi walilalamika kuwa wachuuzi walionekana wakiwauzia wagonjwa wa corona mikate na mayai.

Bw Kyalo alisema kwamba wakazi walihofia usalama wao kufuatia tabia ya wachuuzi kutangamana na wagonjwa. Kulikuwa na ripoti kwamba huenda baadhi ya wagonjwa walikuwa walitoka nje ya kituo kununua bidhaa lakini Bw Kituku alisema hakuna mgonjwa aliyetoka nje ya kituo hicho. “ Nimefahamishwa kuwa ni wachuuzi hao walioingia katika kituo hicho kuuza mayai na mikate,” alisema.

Aliongeza kuwa usalama umeimarishwa katika vituo vyote vya kushughulikia wagonjwa wa corona ili kuhakikisha hali kama hiyo haitatokea tena.

You can share this post!

ODM yakana Raila ana mkataba wa siri na Kalonzo

Juventus wanyakua taji la Serie A kwa msimu wa tisa...

adminleo