• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
Apelekea polisi mkono aliokatwa na nduguye

Apelekea polisi mkono aliokatwa na nduguye

Na CHARLES WANYORO

MAAFISA wa polisi katika kituo kidogo cha Kabachi, Kaunti ya Meru walishangaa mwanamume aliyekatwa mkono alipofika kituoni humo akiwa amebeba mkono huo na kuwataka wauweke vyema kama ushahidi kortini.

Bw Samuel Ndutu, 40, aliambia maafisa wa polisi kwamba alishambuliwa na kaka yake Joseph Ng’olua Jumanne wiki jana kufuatia mzozo wa ardhi.

Alifika kituoni akiwa amebeba mkono huo aliofunga kwenye kitambaa na kuuweka kwenye mfuko wa jaketi lake.

Bw Ndutu alidai kwamba alikatwa kwa upanga alipoenda kukagua shamba lake la miraa katika kijiji cha Leeta, Igembe Kaskazini.

Licha ya kutokwa na damu kwa wingi, mwanamume huyo aliwaendea maafisa wa polisi akiwa mtulivu na baada ya kuwasimulia kisa hicho, aliingiza mkono wake wa kulia kwenye mfuko wa jaketi lake na kuchomoa mkono uliokatwa.

Kisa hicho kilichotokea asubuhi kilivutia maafisa wengi waliokuwa kwenye shughuli tofauti za kikazi kabla ya Mkuu wa Upelelezi wa Jinai (DCI) eneo la Igembe Kaskazini, Benson Omondi kuagiza Bw Ndutu apelekwe hospitali.

Akisimulia kilichotendeka katika hospitali ya wilaya ya Mutuati alipoenda kujaziwa fomu ya polisi ya P3, Bw Ndutu alisema kaka yake alimkabili na kuanza kumgombeza kuhusu ardhi.

Alisema kaka yake alimkimbiza shambani na alipompata alimkata mkono kwenye kiwiko.

Bw Ndutu aliwaomba polisi kumsaka na kumkamata kaka yake ambaye alitoroka baada ya kisa hicho.

Alidai kwamba kaka yake alitisha kumkata mkono uliosalia iwapo ataendelea na kesi dhidi yake.

Bw Richard Mwirigi, 23, kaka yao mdogo alisema kwamba Bw Ng’olua amekuwa akiwatisha na kuwahangaisha jamaa zake nyumbani.

“Anamlaumu Bw Ndutu kwa kunyakua shamba lake. Tumelalamika kwake mara tano lakini haachi kufanya hivyo. Tunachotaka ni haki,” alidai Bw Mwirigi.

Walidai kwamba wazazi wao wanamuunga mkono mshukiwa na sasa wanataka kesi dhidi yake iondolewe na Bw Ndutu ashtakiwe kwa makosa ambayo hawajaeleza.

Visa vya watu kukatwa mikono hutokea mara kwa mara eneo la Igembe.

You can share this post!

Ivanovic avunja kombe la Russsian Cup akilinyanyua

Maddison arefusha mkataba Leicester

adminleo