Makala

TAHARIRI: Viongozi wamalize mzozo wa mgao

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

LEO Jumatatu na kesho Jumanne viongozi wakuu wa vyama vya ODM na Jubilee wanakutana na maseneta wa vyama vyao kuwasisitizia umuhimu wa kupitisha pesa za kutumiwa katika kaunti.

Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), imependekeza mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa kaunti, ambapo kiwango cha pesa kitategemea idadi ya watu katika kaunti badala ya unaotumika sasa ambao unazingatia ukubwa wa eneo.

Ndio sababu kwa sasa, kaunti kama Tana River, Turkana na Marsabit zinapokea kiwango kikubwa cha pesa, japokuwa zina idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na kaunti ndogo kama Kiambu, Nyeri au Nairobi ambazo zina idadi kubwa ya watu.

Mfumo mpya utazingatia watu walio katika kaunti kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya mwaka 2019. Hilo likifanyika, kaunti zilizoko Pwani, baadhi katika maeneo ya Nyanza na Kaskazini Mashariki zitapunguziwa mgao wa fedha.

Jumla ya kaunti 29 zenye idadi kubwa ya watu zitapata mgao wa juu wa Sh316.5 bilioni mwaka wa kifedha wa 2020/21 ikiwa mfumo huo utapitishwa, kama unavyotaka mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta.

Suala hili limeibua mzozo mkubwa, ambao unaonekana kuchochewa kisiasa.

Lengo la kuweka Ugatuzi kwenye Katiba yetu lilikuwa ni kupeleka maendeleo mashinani. Maendeleo na huduma nyingine muhimu hupelekewa watu. Iwapo eneo lina watu wengi, ni wazi kuwa litahitaji pesa nyingi ili kukidhi mahitaji yao.

Kwa mfano, Kaunti ya Nairobi iliyo na zaidi ya watu milioni tano haiwezi kukidhi mahitaji ya wakazi hao na kiwango inachopokea Lamu, Tharaka Nithi au Samburu.

Wanaoshikilia kwamba kaunti zenye ukubwa wa eneo zipewe pesa nyingi, wanakita hoja katika ukweli kuwa sehemu kubwa ya kaunti hizo ni maeneo kame au yaliyosahauliwa kimaendeleo.

Kwamba zikipewa pesa kulingana na ukubwa wake, kutakuwa na maendeleo ya kukaribiana na zile zilizostawi.

Hoja hii haifai kutumika wakati huu, kwa sababu waliounda katiba walizingatia hilo kwa kuweka fedha za usawazishaji (Equalisation Fund). Hazina hiyo, kama haijaanza kutolewa kwa kaunti, ni wajibu wa maseneta na wabunge kupiganie ianze kufanya kazi.

Si busara kutatiza ugawaji raslimali kwa kaunti, kwa kutaka ukubwa wa eneo uzingatiwe, hata kama eneo husika halina watu wa kutosha.