EPL: Aubameyang aongoza Arsenal kuwateremsha Watford daraja
Na CHRIS ADUNGO
WATFORD ambao kwa sasa hawana kocha tangu kufutwa kazi kwa Nigel Pearson mnamo Julai 19, 2020, waliteremshwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika siku ya mwisho ya kampeni za msimu huu wa 2019-20.
Hii ni baada ya fowadi na nahodha wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang kuwafungia waajiri wake mabao mawili na kuchangia moja jingine katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Watford almaarufu ‘The Hornets’ uwanjani Emirates.
Watford walishuka hadi ndani ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho kwa mara ya kwanza mnamo Februari 28, 2020. Walishuka ugani kuvaana na Arsenal wakishikilia nafasi ya 17 jedwalini na ushindi ungaliwaepushia shoka la lililowatema nje ya kampeni za EPL msimu ujao.
Hata hivyo, walianza kipindi cha kwanza kwa utepetevu mkubwa uliowashuhudia Arsenal wakiwafunga jumla ya mabao matatu kufikia dakika 33 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza.
Licha ya kurejea mchezoni katika kipindi cha pili, juhudi zao hazikuzalisha matunda. Badala yake walipoteza mchuano wao wa 20 wa msimu huu na wakaambulia nafasi ya 19 kwa alama 34 sawa na Bournemouth ambao pia walishuka ngazi licha ya kuwapepeta Everton 3-1 uwanjani Goodison Park.
Mbali na Watford na Bournemouth, kikosi kingine kilichoshushwa ngazi kwenye kipute cha EPL msimu huu ni Norwich City waliopokezwa kichapo cha 5-0 kutoka kwa Man-City katika mchuano wao wa mwisho wa muhula huu uwanjani Etihad.
Arsenal walifunga mabao matatu kutokana na majaribio matatu ya kwanza langoni pa Watford. Aubameyang aliwafungulia ukurasa wa mabao kupitia penalti kunako dakika ya tano baada ya beki Craig Dawson kumchezea visivyo fowadi Alexandre Lacazette ndani ya kijisanduku.
Beki mzawa wa Scotland, Kieran Tierney alifanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 24 baada ya kumegewa pasi safi na Aubameyang aliyefunga bao la tatu katika dakika ya 33.
Goli hilo la Aubameyang lilikuwa lake la 22 katika EPL msimu huu. Idadi hiyo ya mabao inawiana na magoli aliyoyafunga katika msimu wa 2018-19 ambao ulimshuhudia akitawazwa mfungaji bora wa EPL kwa pamoja na Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool.
Watford walirejea mchezoni kupitia penalti iliyofungwa na Troy Deeney baada ya beki David Luiz kumchezea visivyo fowadi wa zamani wa Arsenal, Danny Welbeck katika dakika ya 43.
Welbeck, ambaye pia amewahi kuchezea Manchester United, aliwafungia Watford bao la pili katika dakika ya 66. Nusura Welbeck awafungie Watford bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili ila akanyimwa nafasi ya wazi na kipa chaguo la pili la Arsenal, Emiliano Martinez.
Baada ya Bournemouth kuwapepeta Everton 3-1 uwanjani Goodison Park, nao Aston Villa kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United ugani London, hata sare ambayo ingewapa Watford alama moja, isingeweza kuwaepushia shoka la kuwateremsha daraja kutokana na uchache wa mabao yao.
Watford watajilaumu wenyewe kwa maamuzi ya wamiliki wao ambao ni raia wa Italia kuvuruga uthabiti wa kikosi kwa kubadilisha makocha mara tatu katika kampeni za msimu huu.
Pearson alitimuliwa uwanjani Vicarage Road mnamo Julai 19 zikiwa zimesalia mechi mbili pekee licha ya kuwaongoza Watford kujitoa kwenye mduara hatari. Hayden Mullins ambaye ni kocha wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23 aliaminiwa kuwa mshikilizi wa mikoba ya kikosi hicho katika mechi za wiki ya mwisho ya kampeni za muhula huu.
Mechi dhidi ya Arsenal mnamo Julai 26, 2020 ilikuwa ya sita mfululizo kwa Watford kupoteza msimu huu.
Huku msimu mpya wa soka ya Uingereza ukitarajiwa kuanza upya mnamo Septemba 12, 2020, kibarua kikubwa zaidi ambacho kwa sasa wamiliki wa Watford wanacho ni kutafuta mkufunzi mpya atakayewaongoza kurejea katika EPL mwishoni mwa msimu wa 2020-21.
Licha ya kuwa msimu mbovu zaidi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Arsenal walikamilisha muhula wa 2019-20 kwa matao ya juu. Waliambulia nafasi ya nane kwa alama 10 nje ya mduara wa nne-bora huku pengo la pointi 43 likitamalaki kati yao na mabingwa Liverpool waliojizolea alama 99.
Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal kwa sasa watafuzu kunogesha kipute cha Europa League msimu ujao iwapo watawapepeta Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1, 2020 uwanjani Wembley, Uingereza.
Zaidi ya kuwaangusha Chelsea, jingine kubwa zaidi katika maazimio ya Arteta ni kumshawishi fowadi na nahodha Aubameyang kutia saini mkataba mpya na kuwasadikisha Real Madrid kuwapa huduma za kiungo Dani Ceballos kwa kandarasi ya kudumu.
Arsenal pia wana kibarua cha kuweka wazi mustakabali wa kiungo Mesut Ozil anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi uwanjani Emirates tangu atie saini mkataba mpya wa miaka mitatu na nusu mnamo Januari 2018.
Ozil ambaye ni mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani, hajawabishwa na Arsenal katika mechi 10 za mwisho za msimu huu. Aidha, kiungo Matteo Guendouzi ambaye aliwasilisha ombi la kuondoka Emirates tangu azue fujo mwishoni mwa mechi kati ya Arsenal na Brighton mnamo Juni 20, hajawahi kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal.