Michezo

Aston Villa waponea chupuchupu kuteremshwa ngazi kwenye EPL

July 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

ASTON Villa watasalia kunogesha kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao baada ya kuwalazimishia West Ham United sare ya 1-1 katika mchuano wa mwisho wa msimu huu uwanjani London mnamo Julai 26, 2020 na kuponea chupuchupu kuteremshwa ngazi.

Nahodha Jack Grealish aliibuka shujaa wa Villa baada ya kuwafungia waajiri wake bao katika dakika ya 84 ila juhudi zake zikafutiliwa mbali na Andriy Yarmolenko aliyesawazisha sekunde chache baadaye.

Alama hiyo moja iliyotwaliwa na Villa dhidi ya West Ham pamoja na ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Watford uliwasaidia vijana wa kocha Dean Smith kuponea chupuchupu na hivyo kuwaweka Bournemouth katika ulazima wa kuteremshwa ngazi licha ya ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Everton ugani Goodison Park.

Mwishowe, Bournemouth, Watford na Norwich City walipepetwa 5-0 na Manchester City ndio walioshuka daraja kwenye EPL katika msimu wa 2019-20.

West Ham walijipa uhakika wa kusalia ligini msimu ujao mnamo Julai 22 baada ya kuwalazimishia Manchester United sare ya 1-1 uwanjani Old Trafford. Vijana hao wa kocha David Moyes walifunga msimu kwa alama 39 zilizowadumisha katika nafasi ya 16 jedwalini.

MATOKEO YA EPL (Siku ya mwisho ya msimu 2019-20):

Arsenal 3-2 Watford

Burnley 1-2 Brighton

Chelsea 2-0 Wolves

Palace 1-1 Tottenham

Everton 1-3 Bournemouth

Leicester 0-2 Man-United

Man-City 5-0 Norwich

Newcastle 1-3 Liverpool

Southampton 3-1 Sheffield Utd

West Ham 1-1 Aston Villa