TAHARIRI: Ahadi za sukari zisiwe maneno tu
Na MHARIRI
KATIKA siku za hivi majuzi, serikali iliibua ahadi zake kuhusu ufufuzi wa sekta ya kilimo cha miwa na utengenezaji sukari nchini.
Sekta hiyo ambayo ilikuwa tegemeo la kiuchumi hasa kwa wakazi wa maeneo ya Magharibi na Nyanza, imekumbwa na changamoto tele kwa miaka mingi sasa.
Kilimo cha miwa hakina faida ikilinganishwa na ilivyokuwa zamani, kwani viwanda vya serikali vimefilisika huku vile vya kibinafsi vikishindwa kutosheleza mahitaji ya wakulima.
Katika mipango yake, serikali inasema kuna mipango ya kukodisha viwanda hivyo ili vianze kuwa na usimamizi bora, kando na marufuku ya uagizaji sukari kutoka nchi za nje ambayo ni suala linalosababisha hasara kwa wakulima wa humu nchini.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wametilia shaka kujitolea kwa serikali kufufua sekta hiyo licha ya ahadi tele zinazotolewa.
Wasiwasi wa viongozi hao kwamba huenda hizi ni ahadi hewa inaeleweka kwa sababu si mara ya kwanza ambapo tunasikia kuhusu mipango ya kufufua sekta hiyo muhimu.
Katika miaka iliyopita, wakulima walikuwa na matumaini tele walipoambiwa, si mara moja, kwamba madeni ya viwanda vya serikali yalifutiliwa mbali.
Ahadi hii imerejea tena mwaka huu, kwa hivyo mtu yeyote anayefuatilia masuala haya kwa karibu ataona wazi kwa nini ni vigumu baadhi ya wadau kuamini yale wanayoambiwa na serikali.
Isitoshe, imekuwa kawaida ahadi hizi kutokea miaka michache kabla Uchaguzi Mkuu ufanywe.
Serikali inafaa ionyeshe kwa vitendo kujitolea kwake kuondoa changamoto ambazo zinakumba sekta ya kilimo cha miwa na utengenezaji sukari.
Mabwanyenye wanaofaidika kwa kuagiza sukari ya bei rahisi kutoka nchi za kigeni wanafaa kuzimwa mara moja kwa manufaa ya mkulima Mkenya.
Vile vile, ushauri wa wataalamu kuhusu utumizi wa tekinolojia za kisasa katika kilimo cha miwa ufuatwe kikamilifu.
Mojawapo ya sababu zinazofanya tupate sukari ya bei rahisi kutoka nje ni kwa vile tumekataa kukumbatia mbinu za kisasa za kilimo na uzalishaji bidhaa viwandani, ambazo zitasaidia kupunguza gharama za uzalishaji.
Itakuwa bora tuchunguze kitu yanachofanya mataifa yanayouza bidhaa hii kwa bei rahisi kutuzidi sisi ndipo tufahamu yanachofanya kuhusu gharama ya uzalishaji ambayo hatimaye huathiri bei ya sukari.
Viongozi wakome kutumia masaibu ya sekta hii kisiasa kila mara kwani anayeumia ni mkulima mashinani.