Wasaka maiti ya mwanamke aliyezama akipigwa picha
Na STEVE NJUGUNA
POLISI na maafisa wa Shirika la Kenya Red Cross wameungana na wale wa zima moto wa serikali ya kaunti ya Laikipia kutafuta mwili wa mwanamke aliyezama katika mto Ewaso Narok akipigwa picha na kaka yake.
Bi Jemima Oresha alizama Jumapili alipoteleza akipigwa picha na kaka yake katika maporomoko maarufu ya maji ya Thomson Falls mjini Nyahururu.
Iliripotiwa kwamba alikuwa amesimama kwenye jiwe karibu na mto huo ulio sehemu ya chini ya maporomoko hayo alipoteleza na kutumbukia mtoni.
Kulingana na kaka yake, Bw Zablon Mungafu, alikuwa akipiga picha mkasa huo ulipotokea.
Alisema dada yake alikuwa amesafiri hadi Nyahururu kutoka Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia mnamo Jumamosi kuwatembelea jamaa zao wanaoishi mjini humo na alipaswa kurejea Kitale Jumatatu.
“Mnamo Jumapili alisema hangerudi Kitale kabla ya kutazama maporomoko maarufu ya kitalii ya maji ya Thomson Falls,” alisema Bw Mungafu.
Aliongeza: “Tulipofika katika eneo hilo alifurahia kuona maporomoko hayo. Alisema yanavutia na akasisitiza nimpige picha akisimama kwenye jiwe lililo mita mbili kutoka nilipokuwa,” alisema.
Bw Mangafu alisema ni wakati huo ambapo aliteleza na kuingia kwenye maji.
“Nilikuwa nimemaliza kumpiga picha na alikuwa akija nilipokuwa alipoteleza na kuingia mtoni akasombwa na maji nikitazama. Sikuweza kufanya lolote kwa sababu maji yalikuwa yakienda kwa kasi ya juu,” alisema.
Alisema alifahamisha maafisa wa usalama waliokuwa eneo hilo na wakaanza juhudi za kumuokoa. Familia yake inaomba serikali ya kaunti ya Laikipia kutuma wapiga mbizi zaidi kusaidia kuopoa mwili wa binti yao.