Nzoia Sugar sasa kupokea fedha za udhamini baada ya kulegeza msimamo dhidi ya FKF
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha Nzoia Sugar kinatarajia wiki hii kupokea mgao wa sehemu ya Sh13 milioni za kwanza za dili ya udhamini kati ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na kampuni ya kamari ya BetKing kutoka Nigeria.
Hii ni baada ya Nzoia hatimaye kutia saini mkataba wa makubaliano kati ya FKF na BetKing.
Nzoia ni miongoni mwa klabu tatu za Ligi Kuu ya soka ya Kenya ambazo zilitilia shaka mpango wa udhamini wa BetKing na ushirikiano wake na FKF katika mkutano wa wiki jana ulioandaliwa na Rais wa FKF, Nick Mwendwa.
Mnamo Julai 24, klabu 15 kati ya 18 za Ligi Kuu ya soka ya humu nchini zilipokea hundi ya Sh13 milioni ambazo ni malipo ya awali kabisa kutoka kwa BetKing.
Kakamega Homeboyz, Nzoia na mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia hawakupokea mgao wa fedha hizo huku usimamizi wa Gor Mahia ukisisitiza haja ya kuchunguzwa mwanzo kwa mkataba kati ya FKF na BetKing.
Klabu 17 kati ya 18 za Ligi Kuu zilihudhuria mkutano wa FKF ambapo wenyeviti wa vikosi hivyo walikubaliana kuunda kamati maalumu ya kushughulikia uhamisho wa Ligi Kuu ya soka kutoka kampuni ya KPL.
Elly Kalekwa ambaye ni Rais wa Sofapaka, alikosa kuhudhuria mkutano huo ulioshuhudia wenyeviti Dan Shikanda (AFC Leopards), Maoga (Kariobangi Sharks), Daniel Aduda (Tusker), Erick Oloo (Ulinzi Stars) na Ken Ochieng (Zoo Kericho) wakichaguliwa kuwa vinara wa kamati ya mpito itakayosimamia mchakato wa kubadilisha Ligi Kuu ya KPL hadi kuwa Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKFPL).
Wenyeviti Bob Munro (Mathare United), Cleophas Shimanyula (KK Homeboyz) na Evance Kadenge (Nzoia) walipiga kura dhidi ya wenzao watano waliochaguliwa kusimamia kamati ya mpito ya FKFPL.
Wakili Ambrose Rachier ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa KPL hakushiriki kikamilifu mkutano huo. Mbali na kutochangia hoja yoyote wakati wa mkutano huo wa mtandaoni, hakushiriki shughuli ya upigaji kura, kuuliza swali wala kujibu.
Mkataba wa KPL ambao wamekuwa waendeshaji wa Ligi Kuu ya soka ya Kenya, unatamatika rasmi mnamo Septemba 2020. FKF inatarajiwa kufichua mpango mwingine kuhusu udhamini wa soka ya Kenya wiki hii.
Kwa mujibu wa mkataba mpya wa FKF na BetKing ambayo ni kampuni ya mchezo wa kamari, klabu zitalipwa jumla ya Sh13 milioni za mwanzo siku saba baada ya makubaliano. Mwezi mmoja kabla ya kampeni za msimu mpya kuanza, klabu zitapokea Sh75 milioni kisha Sh75 milioni tena baada ya miezi mitatu.
BetKing inatazamiwa kufadhili soka ya Ligi Kuu ya Kenya kwa hadi kiasi cha Sh1.2 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
FKF imethibitisha kuwa mpango huo utashuhudia kila kikosi cha Ligi Kuu ya FKFPL kikipokezwa Sh8 milioni kwa msimu.
BetKing pia imefadhili soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza kwa Sh100 milioni. Mpango huo utaendeshwa kwa miaka mitano ijayo huku kila kikosi kitakachoshiriki kivumbi hicho kikipokezwa Sh500,000 kwa mwaka.
Kadenge ambaye awali alikuwa mkosoaji mkuu wa Mwendwa, amethibitisha kwamba sasa wamewasilishia FKF maelezo muhimu ya akaunti yao ya benki na wanatazamia kupokea mgao wa kwanza wa Sh500,000 kufikia mwisho wa juma hili.
Kwa mujibu wa Kadenge, maamuzi ya Nzoia yalifikiwa baada ya usimamizi wa klabu kusoma kwa kina na kuelewa maafikiano kati ya FKF na BetKing kabla ya kuidhinisha mpango huo wa udhamini.
Kadenge alipokezwa uenyekiti wa Nzoia mnamo Februari 2020 baada ya kuondoka kwa Yappets Mokua. Akihojiwa na mojawapo ya magazeti ya humu nchini, Kadenge alifichua kwamba kwa sasa mipango ya kikosi ni kuisuka upya benchi ya kiufundi ambayo haijakuwa na kocha tangu Mei 2020 baada ya kuondoka kwa Collins ‘Korea’ Omondi. Mikoba iliyoachwa na Korea imekuwa ikishikiliwa kwa muda na Sylvester Mulukurwa.
“Tunalenga kumwajiri kocha aliye na tajriba pevu na uzoefu mpana katika soka ya Kenya. Usimamizi wa klabu unapanga pia kuandaa kikao kitakachoamua ni linin a ni mkufunzi yupi tutakayemsajili japo Mulukurwa ameridhisha na kudhihirisha ukubwa wa uwezo alio nao. Hatuwezi kuajiri kocha wala kusajili wachezaji kwa sasa kwa sababu hatujui ni lini ambapo shughuli za michezo zitarejelewa humu nchini,” akasema Kadenge.