Kimataifa

Hofu watu 60 wakiuawa vita vipya vikianza Darfur

July 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

KHARTOUM, Sudan

ZAIDI ya watu 60 wameuawa katika mapigano mapya yaliyotokea juzi Magharibi mwa Darfur nchini Sudan, maafisa wa Umoja wa Mataifa (UN) wameripoti.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abdalla Hamdok, ameahidi kutuma wanajeshi zaidi eneo hilo.

Takriban wanaume 500 wenye silaha waliwashambulia watu wa jamii ya Masalit, kwa kupora mali yao na kuteketeza nyumba na sehemu ya soko katika mji wa Masteri, kaskazini mwa jimbo la Beida mnamo Jumamosi alasiri, taarifa kutoka afisi ya UN ya kushirikisha utoaji misaada ya kibinadamu (OCHA) ilisema.

“Hii ilikuwa ni moja ya msururu wa visa vya utovu wa usalama vilivyoripotiwa wiki jana ambapo nyumba, masoko na maduka kadha yaliporwa na kuteketezwa huku miundomsingi ikiharibiwa,” taarifa hiyo iliyotolewa na afisi ya OCHA jijini Khartoum ilieleza.

Kufuatia shambulio la Jumamosi mjini Masteri, zaidi ya wenyeji 500 walifanya maandamano wakishinikiza serikali iwape ulinzi.

Mnamo Jumapili, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alisema serikali itatuma vikosi vya usalama katika eneo hilo linalozongwa na vita ili “kuwalinda raia na kuokoa shughuli za kilimo.”

“Kikosi cha pamoja kitatumwa katika majimbo matano ya eneo la Durfur kuwalinda raia wakati huu wa msimu wa shughuli nyingi za kilimo,” afisi ya Hamdok ikasema kwenye taarifa baada yake kukutana na ujumbe wa wanawake kutoka eneo hilo.

Walinda usalama hao watajumuisha wanajeshi na maafisa wa polisi wa kupambana na fujo.

Mnamo Ijumaa, watu wenye silaha walivamia kijiji kimoja na kuwaua raia 20 waliokuwa akirejea mashambani mwao kwa mara ya kwanza baada ya mwaka mmoja, chifu moja aliyeshuhudia kisa hicho aliambia AFP.

Eneo hilo la magharibi mwa Sudan, linalozongwa na umasikini, limeshuhudiwa mapigano ya kikabila kwa miaka mingi. Hali hiyo ilipelekea serikali kuzindua kampeni ya kupambana na wapiganaji hao na kusababisha vifo vya takriban watu 300,000 na wengine 2.5 milioni wakaachwa bila makao.

Hata hivyo, mapigano katika eneo hilo la Darfur yamepungua tangu kung’olewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar el Bashir na wanajeshi, mwaka jana. Hii ni baada ya makundi ya kiraia kufanya maandamano kupinga kupanda kwa gharama ya maisha na utawala mbaya wa kidikteta.

Serikali na muungano wa makundi tisa ya waasi, yakiwemo makundi kutoka Darfur, yalitia saini mkataba wa amani mnamo Januari mwaka huu.

Wakulima ambao walipoteza makao katika mapigano hayo, sasa wameanza kurejelea utayarishaji mashamba yao kwa msimu wa upanzi utakaoanza Agosti na kuisha Novemba 2020.