• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Huenda wageni kutoka nje wasiende karantini – Balala

Huenda wageni kutoka nje wasiende karantini – Balala

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI imetangaza kwamba, huenda ikalegeza kamba kuhusiana na hitaji la wageni watakaotoka nchi za nje kuwekwa kwenye karantini ya lazima ya siku 14.

Hayo yanajiri huku kampuni kadhaa za ndege za kimataifa zikitangaza mipango ya kuanzisha tena safari zao nchini.

Hatua ya serikali kutoweka wageni karantini imenuia kufufua sekta ya utalii ambayo imeathirika pakubwa kufuatia janga na virusi vya corona.

Hoteli nyingi za utalii bado zimefungwa huku wafanyikazi wakiachwa bila ajira na mapato.

Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala alisema Wizara ya Afya itatangaza rasmi msimamo wa serikali kuhusiana na swala la wageni kuwekwa karantini ya lazima lakini akadokeza huenda wageni wakaachwa huru kutembelea maeneo tofauti ya nchi.

“Wizara yetu ya afya itatangaza msimamo wake kuhusiana na swala la karantini kwa wageni wetu…pengine haitatulazimu kuwaweka wageni wetu kwenye karantini ya siku 14 wanapoingia nchini,” alidokeza Bw Balala kwenye mahojiano wikendi.

Hata hivyo wageni hao watalazimika kuwa na vyeti au vibali maalum kutathmini hawana virusi.

“Watakapoabiri ndege watatakiwa kuthibitisha kwamba wamepimwa na wana cheti cha kuonyesha hawana virusi vya corona. Watakapofika humu nchini, tutakuwa na njia zetu za kugundua hilo,” alisema Bw Balala akisisitiza kwamba hatua hiyo itavutia wageni na watalii wengi.

Awali, serikali ilisisitiza kuwa ni sharti wageni hao kuwekwa kwenye karantini ya lazima kwa siku 14 ili kupunguza maambukizi ya virusi hivyo hatari.

Lakini baadaye serikali ilibadili msimamo na kusisitiza kuwa wale wasiokuwa na dalili ya virusi hawatawekwa karantini.

Wawekezaji katika sekta ya utalii walikuwa wamelalamika kwamba hitaji la wageni kukaa karantini litafanya wengi wasitembelee nchini, kwani watapoteza muda ilhali wanataka kutembea Kenya.

Mashirika manne ya ndege za kimataifa ikiwemo KLM, British Airways, Air France na Qatar Airways zimetangaza kwamba wako tayari kuanza safari zao nje na ndani ya Kenya mnamo Agosti 1.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kudai Matiang’i aliugua Covid-19

WANGARI: Mbinu za sayansi ni bora katika kulinda wanyama

adminleo