COVID-19: Visa vipya ni 606 idadi jumla nchini Kenya ikifika 18,581
Na MWANDISHI WETU
VISA vipya vya ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya ni 606 baada ya sampuli 4,888 kufanyiwa vipimo saa 24 zilizopita; Waziri Mutahi Kagwe ametangaza akiwa Afya House, Nairobi Jumanne, visa jumla nchini vikifika 18,581 tangu kisa cha kwanza Machi 13, 2020.
Waziri Kagwe ametahadharisha kwamba Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa maambukizi akitaja eneo ambalo limeanza kuonekana kama kitovu cha janga la corona.
“Eneo la Embakasi jijini Nairobi sasa ni ngome ya Covid-19,” amesema waziri.
Visa vya hivi punde ni 409 jinsia ya kiume huku 197 wakiwa wagonjwa wa jinsia ya kike.
Aidha wagonjwa ni Wakenya 583 nao 23 wakiwa raia wa kigeni.
Waziri amefichua kwamba mgonjwa wa umri mdogo ana umri wa miezi mitano naye yule mkubwa zaidi akiwa na umri wa miaka 85.
Habari njema, Bw Kagwe amesema kwamba watu 75 wamepona wakaruhusiwa kuenda nyumbani na hivyo kufikisha 7,908 idadi ya waliopona maradhi ya Covid-19.
Kenya imefanyia vipimo takriban sampuli 284,500.
Hata hivyo, amesikitika na kutuma salamu za pole kwa familia za watu wengine 14 waliofariki kutokana na Covid-19 na kuifanya 299 idadi jumla ya wahanga.