• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kagwe adai shirika lilitaka kukwepa ushuru wa dawa za HIV

Kagwe adai shirika lilitaka kukwepa ushuru wa dawa za HIV

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, amesema kuwa Shirika la Amerika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) lilikuwa likijaribu kukwepa kulipa ushuru katika uingizaji za dawa za kukabili makali ya virusi vya HIV.

Kumekuwa na mvutano mkali kati ya serikali na shirika hilo kuhusu uingizaji wa dawa hizo nchini, ambazo zimekuwa zikizuiliwa katika Bandari ya Mombasa tangu Januari.

Licha ya serikali kutangaza kuondoa hitaji la shirika kulipa Sh45 milioni kama ushuru, ahadi hiyo haijatekelezwa.Kwenye mahojiano jana, Bw Kagwe alisema kuwa baada ya kubaini hayo, serikali imeanza kuweka masharti makali kuhakikisha kuwa mashirika ya misaada yanayohudumu nchini yanaendesha shughuli zake kwa uwazi.

“Baada ya uchunguzi wetu, tulibaini kuwa USAID ilikuwa ikiingiza dawa hizo nchini kwa kutumia kampuni ya kibinafsi ya Chemonics. Hicho ndicho kimekuwa chanzo cha mvutano uliopo. Ingawa dawa zinalenga kuwasaidia watu wetu, lazima pawe na uwazi katika taratibu zinazofuatwa kuingiza dawa hizo,” akasema Bw Kagwe.

Utata huo unaendelea kuhatarisha maisha ya zaidi ya Wakenya 1.2 milioni ambao hutegemea dawa hizo kupunguza makali ya virusi hivyo.Huku serikali ikishikilia kuwa shirika hilo lilitumia njia za “kijanja” kuingiza dawa nchini, shirika hilo nalo linashikilia kuwa halitakubali dawa hizo zisambazwe nchini na Halmashauri ya Kusambaza Dawa Kenya (Kemsa) kutokana na tuhuma za ufisadi zinazoikabili.

Kemsa imejipata katika utata baada ya mabilioni ya pesa kupotea katika hali tatanishi kwenye utoaji kandarasi za ununuzi wa vifaa vya kuisaidia Kenya kukabili virusi vya corona mwaka uliopita.

Mwezi uliopita, Bw Kagwe aliliambia Bunge la Taifa kuwa USAID italazimika kusambaza dawa hizo kwa kutumia utaratibu ambao serikali imekuwa ikitumia kusambaza dawa zingi.

Wakati huo huo, Bw Kagwe amesema kuwa serikali itaanza mkakati maalum kwa ushirikiano na vyama vya wahudumu wa matatu na wahudumu wa bodaboda kuhakikisha kila mmoja ana bima inayomlinda kuhusiana na masuala kama ajali.

Alieleza kuwa Wakenya wengi wamekuwa wakiteseka sana kutafuta matibabu hasa baada ya kupata ajali, kwani wengi huwa hawana bima maalum za afya.Alisema ni kinaya kuwa magari mengi huwa na bima hizo ilhali waendeshaji hawana.

You can share this post!

28,000 waliozoa ‘E’ KCSE bado wana fursa ya...

Wanafunzi wawili wa MKU wapata ufadhili kwa ubunifu wao...