• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
GWIJI WA WIKI: Michael Muingi

GWIJI WA WIKI: Michael Muingi

Na CHRIS ADUNGO

KUKWEA ngazi za maisha kunastahili nidhamu na uvumilivu.

Hakuna mafanikio utakayoyapata bila ya kujituma. Zoea kuangusha jasho ndipo upate!

Maamuzi yoyote unayoyafanya maishani ni zao la agano kati ya nafsi na mawazo yako. Jiamini, jikubali na ukatae maisha ya kujihukumu. Anayeongozwa na imani ndiye hufaulu!

Jitahidi kufanya vizuri ili hatimaye uiache dunia. Ukijitahidi kufanya vibaya, ni dunia itakayokuacha.

Mungu akikupa kipaji, kitumie vyema kwa lengo la kuwafaidi wengine bila ya kujali sana malipo.

Ukamilifu katika maisha hutegemea mchango wa marafiki wanaokuzingira. Wateue wasiri wako kwa makini na upime sana mizani ya maisha!

Huu ndio ushauri wa Bw Michael Muingi – mwandishi mzoefu, mshairi shupavu, mtahini stadi, mlezi wa vipaji na mwalimu wa Kiswahili ambaye kwa sasa ni naibu mwalimu mkuu na msimamizi wa masuala ya kiakademia katika shule za KBA Group of Schools, Kahawa West, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Muingi alizaliwa mnamo 1983 katika mtaa wa Magongo, eneo la Kaloleni, Kaunti ya Mombasa. Yeye ni mwana wa tatu katika familia ya watoto wanane wa Bw Francis Muingi na Mwalimu Susan Mbula. Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Magongo alikosomea kati ya 1990 na 1994. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya Kyuasini babaye mzazi alipopata uhamisho wa kazi hadi Kaunti ya Makueni mnamo 1995.

Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika mwaka wa 1997.

Alama nzuri alizozipata zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Makueni Boys. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2001.

Ingawa matamanio yake yalikuwa ni kuhudumu katika Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF), Muingi alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Highridge, Nairobi alikosomea kati ya 2003 na 2005.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Shahada ya Elimu (Kiswahili na Jiografia) kati ya 2012 na 2016. Alijisajilisha baadaye kwa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta na anatazamia kufuzu mwishoni mwa mwaka huu chini ya usimamizi na uelekezi wa Dkt Richard Makhanu Wafula na Dkt Timothy Arege.

Kati ya mambo yaliyochangia umilisi wake katika Kiswahili ni ulazima wa kuitumia lugha hii kuwasiliana na watu wa jamii na matabaka mbalimbali jijini Mombasa.

Muingi anatambua pia mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza ipasavyo, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali, kumshajiisha maishani na kumhimiza kujitahidi masomoni.

Mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa mara kwa mara na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.

Guru ndiye alimpigia mhuri wa kuwa mwalimu bora wa Kiswahili na kumpa motisha ya kupiga mbizi katika bahari ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili.

Mwalimu Mwenzwa wa Shule ya Msingi ya Kyuasini ndiye alitambua kipaji cha Muingi katika utunzi wa kazi bunilizi. Sanaa hiyo ilikuzwa sana ndani yake na Mwalimu Jara wa Makueni Boys aliyemtia ari ya kukichangamkia Kiswahili kwa kani na idili.

Ilhamu zaidi ya Muingi katika kukichapukia Kiswahili ilichangiwa na wanafunzi wenzake wa shule ya msingi waliompagaza jina Mswahili Kamili kwa upekee wa lafudhi yake kila alipoyaita na kuyatema maneno ya lugha hii.

UALIMU

Baada kukamilisha mtihani wa KCSE, Muingi alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Kyuasini kati ya 2002 na 2003.

Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na mazingira faafu yaliyomwezesha kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Alirejea kufundisha shuleni humo baada ya kuhitimu rasmi kuwa mwalimu mnamo Agosti 2005. Aliaminiwa fursa ya kuwaelekeza watahiniwa wa KCPE mwaka huo. Matokeo bora yaliyoandikishwa na wanafunzi wake kitaifa yaliwavutia zaidi wasimamizi wa Shule ya Msingi ya KBA waliomtwaa mwanzoni mwa 2006 na kumfanya Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Tangu mwaka huo, Muingi amehudumu KBA akishikilia nyadhifa mbalimbali. Aliteuliwa kuwa Mwalimu Mwandamizi mnamo 2008 kabla ya kuwa Naibu Mwalimu Mkuu mwanzoni mwa 2010.

Yeye kwa sasa ndiye msimamizi wa masuala yote ya kiakademia katika KBA Group of Schools.

UANDISHI

Japo sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani ya Muingi akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi, safari yake katika ulingo huu ilianza rasmi mnamo 2005.

Ametunga idadi kubwa ya mashairi ya kizalendo ambayo yamekuwa yakifana na kutia fora katika tamasha za kitaifa za muziki. Mashairi hayo anayoyatunga kwa ufundi mkubwa, yamewahi pia kumpandisha kwenye majukwaa mbalimbali ya tuzo za haiba kubwa. Aliwahi kutunga shairi ambalo wanafunzi wake wa KBA walimkariria Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Mombasa mnamo 2014.

Muingi ndiye mtunzi wa shairi Mvua Hii lililowahi kumvunja mbavu Rais Kenyatta lilipokaririwa na mwanafunzi Emily Wanjiru wa Shule ya Gachororo ECD Ruiru katika Ikulu ya Sagana mnamo 2014.

Muingi amekuwa pia mtunzi mzoefu wa misururu ya Mitihani ya Mentor, Waka na Darubini ya KCPE ambayo hutegemewa pakubwa na zaidi ya shule sabini za msingi katika kishada au eneo pana la Kasarani, Nairobi.

Baada ya kuchapishiwa msururu wa CRE Revision Darasa la 4-6 mnamo 2013, kampuni ya Champion Publishers ilimfyatulia Muingi vitabu Bingwa wa Marejeleo ya KCPE Kiswahili (2015) na Bingwa wa Marejeleo ya Insha (2016).

Muingi aliwahi pia kutafsiri kwa Kiswahili kitabu The Forgotten Seed hadi Mbegu Iliyosahaulika. Kitabu hicho kilichapishwa nchini Uganda mnamo 2010.

Kwa sasa anaandaa ‘The Mentor Atlas for Primary Schools ambayo itatolewa na Mentor Publishers kufikia Septemba 2020.

Analenga pia kuchapisha diwani ambazo anaamini zitakabadilisha sura ya kufundishwa na kusomwa kwa Ushairi wa Kiswahili miongoni mwa walimu na wanafunzi wa shule za msingi, upili na vyuo.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, kubwa zaidi katika maazimio ya Muingi ni kuwa Mhadhiri wa Kiswahili katika kimojawapo cha vyuo vikuu vya Ujerumani.

Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii.

Muingi anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo Kiswahili na warsha za kuelekezana, kushauriana na kuhamasishana kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCPE.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Muingi hujishughulisha pia na kilimo cha pojo na ufugaji wa nyuki katika Kaunti ya Makueni

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Kisa cha Mlajasho mfano kwa vijana

Kenya ina PPE za kutosha, asema Kagwe

adminleo