Makala

TAHARIRI: Vijana wanahitaji mipango ya kudumu

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

SERIKALI inahitajika kuwazia jinsi itakavyosaidia maelfu ya vijana kitaifa wanaohusika katika mpango wa Kazi Mtaani kwa muda wa kudumu.

Jumla ya Sh10 bilioni zilikuwa zimetengwa kwa mpango huo, ambapo vijana hutakikana kufanya kazi za kusafisha mitaa kisha wanalipwa kiasi kidogo cha fedha ili kuwakimu katika nyakati hizi ngumu za janga la corona.

Ijapokuwa kuna changamoto kadha ambazo zimeshuhudiwa kufikia sasa, kama vile malalamishi ya majina ya baadhi ya vijana kukosekana wakati wa malipo, na malipo kuchelewa, mpango huo, ukitekelezwa vyema utasaidia katika kipindi hiki cha matatizo mengi.

Hata hivyo, tusisahau kwamba kuna wakati janga la corona litatatuliwa, pengine tiba kamili au chanjo itakapopatikana.

Kwa msingi huu, ni lazima wadau wote wanaohusika katika mpango huo wafikirie kuhusu hatima ya vijana ambao kwa sasa wamepata vibarua katika Kazi Mtaani.

Kuna baadhi yao ambao walikuwa na ajira au vibarua kwingine, na pengine watarudia kazi zao wakati hali ya kawaida itakaporudi.

Lakini wakati huo huo, kuna wengine wengi ambao hawakuwa na mbinu zozote za kujitafutia riziki na sasa wamebahatika, kando na wale ambao huenda hawatanufaika kurudia kazi zao za awali.

Hiki ni kikundi cha vijana ambao serikali inafaa iweke mikakati ya kutosha ili pia baadaye waendelee kupata riziki kwa njia ya haki.

Kuna mipango mingi ambayo imewahi kupitishwa katika miaka iliyopita kwa lengo la kunufaisha vijana, kama vile hazina za kuwapa mikopo kirahisi ili waanzishe biashara.

Mipango hiyo yote haikufanikiwa kuondolea nchi hii janga la ukosefu wa ajira kwa vijana licha ya mabilioni ya pesa ambazo zilitumiwa.

Changamoto zilizoibuka katika mipango hiyo yote, pamoja na yale yanayoonekana katika mpango wa Kazi Mtaani, zitumiwe kama mafunzo yatakayotoa mwongozo wa kusaidia vijana katika miaka ijayo.

Hakutakuwa na faida yoyote serikali ikitumia mabilioni ya pesa kila mara kwa lengo la kunufaisha vijana, kisha malengo makuu yanakosa kutimizwa kwa sababu wadau walirudia makosa ambayo yalikuwa yametendeka katika mipango ya awali.

Zaidi ya hayo, mpango wowote unaolenga vijana haupaswi kutekelezwa kiholela bila kujumuisha maoni yao.