Habari

Corona yavuruga maandalizi ya Idd-ul-Adha

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MISHI GONGO na VALENTINE OBARA

SHUGHULI chache zilishuhudiwa Jumatano wakati Waislamu walianza kujiandaa kwa sherehe za Idd-ul-Adha ambazo zitafanyika Ijumaa.

Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i alitangaza rasmi kwamba Ijumaa itakuwa ni sikukuu ya kitaifa ili kutoa nafasi kwa Waislamu nchini kufanikisha sherehe hizo muhimu.

Kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19 kimataifa, Waislamu waliohojiwa na Taifa Leo walisema hawatakuwa na uwezo wa kusherehekea jinsi ilivyokuwa kawaida katika miaka iliyopita.

Kawaida siku tatu kabla ya sherehe hiyo, Waislamu hufurika katika masoko mbali mbali kujinunulia bidhaa kama nguo, vyakula na mnyama wa kuchinja. Hata hivyo, mwaka huu makumi tu ya waumini ndiyo wanaonekana sokoni walifanya matayarisho

Sikukuu hiyo ambayo husherehekewa kila mwaka baada ya ibada ya Hijja mjini Mecca, huhusisha waumini hao kuchinja mfugo wa miguu minne kwa kumbukumbu ya Nabii Ibrahim aliyekuwa ameagizwa kumchinja mwanawe Ismael.

Dhul Hijja, ambao ni mwezi wa kumi na mbili na wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu, huonekana kwa wengi kama nafasi ya kuimarisha imani yao.

Katika soko la Kongowea na Marikiti, Kaunti ya Mombasa, waumini waliojitokeza kununua bidhaa, walilalamikia ukosefu wa fedha.

Bi Salma Mzee, aliyekuwa akichagua nguo katika soko la Marikiti, alisema uhaba wa fedha umemfanya kupunguza mahitaji ya siku hiyo.

“Kila mwaka mimi huwanunulia wanangu wanne nguo tatu kila mmoja lakini mwaka huu nimewanunulia nguo moja tu. Nilikuwa nafanya biashara ya kuuza chakula lakini kwa sasa imesimama,” akasema.

Bw Yusuf Hamza ambaye ni muuzaji nguo katika soko hilo alisema mauzo katika mwaka huu yamekuwa chini mno.

“Idd-ul- fitri hakukuwa na biashara kufuatia sehemu hii kufungwa ili kudhibiti maambukizi, tulitegemea sikukuu hii mambo yatabadilika lakini biashara imezorota kabisa,” akasema.

Muuzaji mwengine Ahmed Zakir alisema wengi wanaofika katika soko hilo wananunua madera.

“Dera ni Sh250 pekee, wanawake wengi wanakimbilia urahisi hakuna anayenunua magauni hata watoto wananunuliwa madera,” akasema.

Bw Abdullah Ali anayeuza mbuzi, alisema hadi kufikia sasa ameuza mbuzi 40 tu, kinyume na hapo awali ambapo nyakati kama hizi angekuwa ameuza zaidi ya mbuzi 100.

Kutokana na kuwa uchinjaji ni jambo muhimu wakati wa sherehe hizo, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitoa mwongozo kuhusu jinsi familia zinavyoweza kufanikisha jambo hilo bila kujihatarisha kueneza virusi vya corona.

Katika mwongozo huo, WHO ilipendekeza maafisa waongeze sehemu za uchinjaji mifugo ili shughuli hiyo isifanywe manyumbani, bali katika sehemu ambapo kuna hakikisho la usalama.

Shirika hilo lilihimiza kuwe na usafi wa hali ya juu vichinjioni, na pia katika masoko ambapo watu wengi watatarajiwa wakati huu.

WHO pia ilipendekeza kuwa, usambazaji wa misaada kwa jamii usifanywe na makundi kiholela bali kuwe na mashirika ambayo yatakusanya misaada hiyo na kuisambaza.

Mwongozo huo ulizidi kusema mapendekezo hayo yanafaa kufuatwa pamoja na mengine ambayo tayari yametolewa kwa minajili ya kuepusha ueneaji wa virusi vya corona.