• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
COVID-19: Viongozi wawashauri Waislamu watii masharti wakati wa sherehe za Idd kuu

COVID-19: Viongozi wawashauri Waislamu watii masharti wakati wa sherehe za Idd kuu

CECIL ODONGO na MOHAMED AHMED

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (Supkem) limewataka waumini wote washerehekee Sikukuu ya Idd-ul-Adha kwa kuzingatia masharti yote yaliyotolewa na serikali kama hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado amewataka Waislamu waswali nyumbani na pia wajizuie kujikusanya kwenye makundi kutokana na hatari iliyopo ya kupata Covid-19.

Idd kuu ya mwaka 2020 inasherehekewa wakati ambapo waumini wengi hawakuenda Hija mjini Mecca kwa sababu ya changamoto za corona.

Saudia pia ilizima usafiri wa ndege nje na ndani ya taifa hilo kutokana na janga hilo.

“Tunawaomba Waislamu watumie nafasi iliyopo kusheherekea Idd kwa kuzingatia masharti yote ya Wizara ya Afya. Tunashauriwa kujizuia kujikusanya, kuvaa barakoa kila mara, kuosha mikono kwa kutumia sabuni na sanitaiza na kuzingatia umbali wa mita moja unusu,” akasema Bw Naado kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Pia alimshukuru Rais Rais Uhuru Kenyatta kwa kutenga siku ya leo kama sikukuu na kuwaruhusu Wakenya wapumzike.

Wakati uo huo misikiti mbali mbali neo la Pwani imetoa mwelekeo wa jinsi swala litaendeshwa bila kukongamana viwanjani jinsi ilivyokuwa mwaka jana kabla ya ujio wa virusi vya corona.

Kaunti ya Mombasa ambayo ni ya pili kwa idadi ya maambukizi ya corona, imepiga marufuku mikusanyiko ya watu na swala limeruhusiwa misikitini pekee au mtu binafsi kushiriki ibada nyumbani kwake.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na mkuu wa afya ya umma katika kaunti ya Mombasa Dkt Aisha Abubakar, marufuku hayo ni kufuatia hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Tumepiga marufuku hatua hiyo ili kuwalinda waumini kutokana na kuambukizana virusi vya corona,” ikasema taarifa hiyo.

Miongoni mwa masharti ya kuswali msikitini ni waumini wasiozidi 100 kutekeleza ibada kwa muda wa saa moja pekee

Naibu mwenyekiti wa Supkem Sheikh Muhdhar Hitamy aliwahimiza waumini wazingatie usalama wao wa kiafya wanaposwali misikitini

Katika kaunti ya Kwale, kamati ya msikiti wa Jamia ilisema kuwa wataswali katika uwanja wa Baraza park kuanzia saa mbili hadi saa tatu asubuhi. Hata hivyo, ni watu wachache tu wataruhusiwa kuingia huku wakishauriwa washike udhu au kujitawadha nyumbani.

“Watakaobeba mswala mkubwa wa kutumika na watu zaidi ya mmoja wahakikishe utawatosha wakisimama umbali wa mita moja unusu,,” ikasema notisi hiyo.

Waumini pia watapimwa joto kabla kuingia uwanjani huku wazazi wa watoto wadogo wenye umri wa miaka 13 na chini wakiambiwa wasifike nao uwanjani humo.

You can share this post!

Mahakama yaamuru mbunge Alice Wahome arudishiwe walinzi

Mahakama yaagiza SABIS® International ipunguze karo kwa...

adminleo