Makala

TAHARIRI: Elimu: Serikali sasa ijirekebishe

July 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

PENDEKEZO la Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, hapo Alhamisi kuhusu mbinu mpya ya kufunza watoto wasioweza kupokea elimu kwa mitandao, ni tatizo lililochangiwa na serikali yenyewe.

Ingawa ni hatua nzuri inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanarejelea masomo bila kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona, hili halingekuwepo ikiwa serikali ingeweka miundomsingi ifaayo kuimarisha huduma za mitandao shuleni.

Moja ya ahadi kuu ambazo serikali ya Jubilee ilikosa kutekeleza, ni kuwanunulia wanafunzi wa Darasa la Kwanza vipakatalishi mara tu baada ya kuchukua uongozi mnamo 2013.

Kwenye kampeni zao, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto waliahidi hiyo ndiyo ingekuwa hatua ya kwanza, kwani dunia inaelekea kwenye mfumo wa kidijitali.

Ni ahadi iliyozua msisimko wa aina yake nchini, na iliyojenga matumaini kwa mamilioni ya Wakenya kwamba hatimaye mfumo wa masomo ungebadilika kabisa.

Ni ahadi ambayo pia iliifanya serikali kupewa msimbo wa “Serikali ya Kidijitali”.

Hata hivyo, matumaini ya mamilioni ya wanafunzi yalianza kuvunjika wakati iliibuka mpango huo ulikuwa umegeuzwa kuwa sakata ya uporaji wa mamilioni ya pesa kwa manufaa ya watu wachache waliopewa jukumu la kuusimamia.

Hali ilizidi kudorora wakati serikali ilitangaza kuwa badala ya vipakatalishi, ingetoa tabuleti. Hilo pia halikufaulu kutokana na matatizo yayo hayo.

Bila shaka, tungekuwa tumepiga hatua kubwa ikiwa mpango huo ungefanikishwa tangu 2013.

Hili lingehakikisha wanafunzi wote walio katika shule za msingi za umma, wangekuwa na mitambo hiyo, kwani mwanafunzi aliyekuwa katika Darasa la Kwanza mwaka huo yuko katika Darasa la Nane kwa sasa.

Hivyo, wanafunzi wote walio katika shule za umma wangekuwa na ushindani sawa na wenzao walio katika shule za upili kwenye mfumo wa masomo kupitia mtandao.

Bila shaka, haya ni masaibu yaliyochangiwa na kutowajibika kwa serikali kupitia watu inaowapa kazi kutekeleza ama kusimamia mipango yake.

Kwa Rais Kenyatta, huu ni wakati mwafaka kufufua upya mpango huo ili kuhakikisha wanafunzi nchini wako katika kiwango sawa kimasomo na wenzao katika nchi zilizostawi kiuchumi.