• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
RIPOTI: Ugatuzi bado unawapiga chenga vijana

RIPOTI: Ugatuzi bado unawapiga chenga vijana

Na CAROLYNE AGOSA

ASILIMIA 60 ya vijana nchini hawafahamu jinsi mfumo wa ugatuzi unavyofanya kazi wala majukumu ya viongozi wao wa kaunti.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya utafiti kuhusu hali ya vijana nchini na changamoto kuu zinazowakumba.

Katika utafiti huo ulioagizwa na vuguvugu la vijana la JIACTIVATE, na kuendeshwa na shirika la kimataifa la utafiti la Geo Poll, vijana walitaja changamoto hizo kama: ufisadi, ukosefu wa kazi, huduma za matibabu na ukosefu wa chakula cha kutosha.

Ni miaka mitano tangu mfumo wa ugatuzi kung’oa nanga nchini na vile vile kuundwa kwa serikali za kaunti.

Hata hivyo, ni bayana kwamba idadi kubwa ya vijana hawana ufahamu wa utendakazi wake.

“Karibu asilimia 40 ya waliohojiwa hawaelewi maana sahihi ya mfumo wa ugatuzi. Wengine asilimia 23 hata hawajui ugatuzi ni nini na majukumu ya viongozi waliochaguliwa katika mfumo huo,” ilisema ripoti hiyo ya utafiti uliofanywa katika kaunti 37.

“Kuna mwanya mkubwa sana katika ufahamu wa vijana kuhusu mfumo wa ugatuzi: nini maana yake, unavyofanya kazi, manufaa yake. Vile vile, vijana hawana uwakilishi wa moja kwa moja katika nyadhifa za uchaguzi (za ugatuzi) wala kuwa katika majukwaa yanayowapa usemi,” iliongeza ripoti hiyo iliyozinduliwa Ijumaa mjini Nairobi.

Vijana zaidi ya 1282 – wavulana 774 na wasichana 451 – walishiriki kutoka maeneo ya Nairobi, Kati, Mashariki, Rift Valley, Magharibi, Nyanza, Mashariki Kaskazini na Pwani.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Mei 2017 na Aprili 2018 unaashiria changamoto kubwa inayolikumba taifa la Kenya katika kufanikisha ugatuzi, ikizingatiwa vijana ndio wengi zaidi nchini.

Takriban asilimia 80 ya watu nchini wako chini ya umri wa miaka 35 – kumaanisha kati ya idadi ya jumla ya watu 46 milioni vijana ni 36.8 milioni.

Utafiti ulipata kuwa zaidi ya nusu ya vijana (asilimia 56) wako tayari kuwashinikiza viongozi wao kuwajibika.

Hata hivyo, asilimia 44 walisema hawawezi kutekeleza wajibu huo kwa sababu mbalimbali. Kuu miongoni mwao ni viongozi hao hawapatikani mashinani (asilimia 33), hakuna uwazi na uwajibikaji (asilimia 26) na kukithiri kwa ufisadi (asilimia 18).

Ni jambo litakalowafanya waundaji sera kukuna vichwa vyao ikizingatiwa nusu ya wapiga kura wote 19 milioni nchini ni vijana wenye umri wa miaka kati ya 18 na 35.

 

Vibarua

Kuhusu suala la ajira nchini, asilimia 21.2 ya vijana waliohijiwa wanafanya vibarua ili kukimu mahitaji yao. Asilimia 10.4 wanamiliki biashara huku wengine 9.7 wakiwategemea wazazi ama jamaa zao.

Inakisiwa jumla ya vijana 3.68 milioni hawana kazi – hii ikiwa ni nusu ya Wakenya 7 milioni wasio na kazi.

Kulingana na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), idadi kubwa ya vijana wasio na kazi (asilimia 19.2) ni wenye umri wa kati ya 20 – 24.

Takriban vijana 700,000 hujiunga na sekta ya ajira kila mwaka. Hata hivyo, wengi wanajipata wakifanya kazi zisizoambatana na ujuzi waliosomea chuoni, kazi ambazo zinaweza kufanywa na wale waliofika kidato cha nne.

Vijana wanahofu kwamba watakosa nafasi chache za kazi wanazopewa kwa sababu ya kukosa ujuzi.

Ilieleza ripoti: “Takriban asilimia 13 ya waliohojiwa walisema kuna haja ya kuwapa vijana ujuzi wa biashara na kiufundi.

“Asilimia 28.3 walihimiza vijana kuingilia biashara kama njia mbadala ya ajira huku wengine asilimia 10.1 wakihimiza kilimo kama njia ya kuunda nafasi zaidi za kazi katika jamii zao.”

Utafiti huo wa JIACTIVATE ulifanywa kwa ushirikiano na mashirika mengine ikiwemo Siasa Place, Shirika la Msalaba Mwekundu, Organization of African Youth, Maisha Youth, Youth Clan, Shujaaz na Well-told Stories.

You can share this post!

NTV kuwapa raha mashabiki kwa kuonyesha mechi za Kombe la...

Ajenda Nne Kuu: Kijana airai serikali imkubalie azindue...

adminleo