• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Wafurika misikitini kusherehekea Idd

Wafurika misikitini kusherehekea Idd

MISHI GONGO na WACHIRA MWANGI

WAUMINI wa dini ya Kiislamu hapo Ijumaa walifurika katika misikiti mbalimbali nchini kutekeleza swala ya Idd-ul- Adha.

Katika Kaunti ya Mombasa, Waislamu ambao walikuwa na bashasha kujumuika kwa swala hiyo, hawakujali mvua iliyonyesha.

Sikukuu hiyo iliadhimishwa na waisilamu dunia nzima wakati ambapo janga la corona lingali linatatiza kimataifa.

Waumini wengi waliridhishwa kwa vile walikosa swala ya Idd-ul-fitri kwani wakati huo misikiti ilikuwa imefungwa na serikali.

“Idd iliyopita hatukuswali, lakini twashukuru tumeweza kujumuika katika Idd hii,” akasema Bw Jamal Adnan, muumini aliyekuwa amehudhuria swala hiyo katika msikiti wa Baluchi.

Alisema japo hawakuweza kuswali uwanjani kama ilivyo ada kufuatia agizo kutoka kwa wizara ya afya ya mji huo, walifurahia kutekeleza ibada hiyo msikitini.

Sikukuu ya Idd-ul-Adha ni kilele cha ibada ya Hajj inayofanyika mwezi wa 12 katika kalenda ya Kiislamu.

Mwaka huu watoto wa chini ya umri wa miaka 13 na wazee waliagizwa kusalia nyumbani kufuatia wao kuwa miongoni mwa kundi la watu walio katika hatari kuu ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Mwaka 2020 kila msikiti ulilazimika kuruhusu waumini 100 pekee.

Pia walihakikisha kila mmoja amevalia maski na amebeba mswala wake.

Kadhi mkuu nchini sheikh Ahmed Muhdhar aliwahimiza Waislamu kuendelea kufuata masharti yaliyowekwa kudhibiti ugonjwa huo hadi pale utakapoisha nchini.

Aliwaonya waumini hao dhidi ya kukongamana na kutembeleana akisema kuwa hali hiyo itawaweka Katika hatari ya maambukizi.

Sheikh Fuad Ali aliyekuwa amehudhuria msikiti wa Othman Ibn Afan eneo la Serani, Mombasa alisema ni faraja kwa waumini wa Kiislamu kuweza kutekeleza tena ibada zao msikitini.

Hali tofauti ilishuhudiwa katika Kaunti ya Mandera ambapo waumini wengi walikiuka kanuni za kupambana na corona walipojitokeza kwa swala.

Katika Msikiti wa Jamia ulio mjini Mandera, waumini walianza kufurika msikitini saa kumi na mbili asubuhi.

Sheikh anayehudumu katika msikiti huo alisema maafisa wa serikali waliwaruhusu kufanya ibada kwa sharti tu kuwa kila mtu angevaa barakoa.

Alifichua kuwa walionywa kutoruhusu wanahabari kushuhudia yaliyokuwa yakiendelea.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Mandera, Bw Jeremiah Kosian alisema ingawa viongozi wa Kiislamu waliomba ruhusa kuruhusiwa waswali kwa wingi msikitini, hawakupewa ruhusa.

Karibu misikiti yote mjini ikiwemo Elwak, Banisa, Rhamu na Takaba ilikuwa na idadi kubwa ya watu.

  • Tags

You can share this post!

Ruto awataka maseneta waandae mfumo ‘rafiki’ wa...

Juve wapoteza mechi ya kwanza tangu 2018

adminleo