Wachina watoroka corona Kenya
VALENTINE OBARA na SALATON NJAU
MAMIA ya raia wa China jana Ijumaa walianza kuondoka Kenya kurudi nchini mwao, wakihofia kuambukizwa virusi vya corona.
Waliohojiwa walikiri kwamba, uamuzi wao kuondoka Kenya unatokana na idadi kubwa ya maambukizi yanayoendelea kuongezeka kwa kasi kila siku.
Wengi wao walifichua kuwa, walikuwa wamepanga kuondoka Kenya mapema lakini ubalozi wa China nchini ukapinga ombi lao.
Mapema mwezi uliopita, ilibainika Wachina 400 walipata agizo la Mahakama Kuu ya Nairobi kulazimu serikali iwaruhusu kuondoka nchini, kwani kulikuwa na marufuku ya safari za ndege kutoka Kenya.
Katika kesi hiyo, walikuwa wameeleza wasiwasi kuwa hawana imani Kenya ina uwezo wa kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona ipasavyo.
Jana, idadi kubwa ya waliokuwa wakiondoka ilikuwa ni wanawake na watoto, huku wanaume wengi wakiamua kubaki ikizingatiwa kuna kazi wanazoendelea kufanya humu nchini.
Hata hivyo, serikali ilisema kuondoka kwao ni jambo la kawaida.
Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, alisema hakuna jambo lolote fiche kuhusu Wachina walioamua kurudi kwao.
“Hatujui sababu halisi ya uamuzi wao kuondoka nchini lakini nadhani ni safari ya kawaida tu kwa raia wa kigeni kurudi kwao nyakati kama hizi. Pia sisi tunarudisha Wakenya kutoka nchi nyingine za nje,” akasema.
Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw Solomon Kitungu, alithibitisha kuwa safari hiyo ilikuwa imepangwa mapema.
Katika miezi iliyopita, raia wa nchi nyingine kama vile Uingereza, Italia na Amerika pia yalihamisha raia wao kadha kutoka Kenya.
Wawili hao walikuwa wakizungumza wakati serikali ilitangaza kuwa watu 773 walipatikana wameambukizwa virusi vya corona, na kufikisha idadi ya jumla hadi 20,636.
Katika takwimu alizotangaza, Bw Kagwe alisema watu 44 walipona na hivyo basi idadi yao sasa imefika 8,165. Hata hivyo, wengine 16 walifariki na kufikisha idadi hiyo hadi 341.
Safari ya Wachina kutoka nchini ilitokea siku moja tu kabla Kenya kufungua mipaka yake kwa wageni kutoka mataifa ya kigeni.
Mnamo Alhamisi, Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alitangaza nchi 11, ikiwemo China, ambazo wasafiri kutoka huko watakubaliwa kuingia nchini.
Jana alifafanua kwamba, orodha hiyo ni ya nchi ambazo wasafiri hawatahitajika kwenda karantini wakifika Kenya kama hawana dalili za Covid-19.
Mataifa mengine yaliyoruhusiwa ni Korea Kusini, Japan, Canada, Zimbabwe, Ethiopia, Uswisi, Rwanda, Uganda, Namibia na Morocco.
Bw Macharia aliongeza mataifa mengine kwenye orodha hiyo jana ikiwemo Amerika, Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani, Uholanzi, Qatar na Milki ya Uarabuni (UAE).
Bw Kagwe alisema orodha hiyo ambayo itakuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara, haifai kuchukuliwa kuashiria hali ya uhusiano wa Kenya na mataifa ambayo hayamo.
Kilichovutia wengi ni jinsi Amerika na Tanzania hazikujumuishwa katika orodha ya kwanza.
“Kanuni za usafiri wakati huu si suala la uhusiano wa kidiplomasia bali zinatolewa kwa hitaji la kulinda afya ya umma. Matakwa yanayogusia kila nchi yatakuwa yakibadilishwa mara kwa mara kwa kuzingatia hali itakavyokuwa,” akasema.
Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Koki Mutua, alieleza kuwa serikali itaarifu wasafiri wanaotoka nchi za nje kuhusu mtandao ambao watahitajika kutumia kujaza maelezo kuwahusu kabla waanze safari.
Katika mtandao huo maalumu, kila msafiri atatakikana kujaza maelezo yake ikiwemo anwani zake, kisha kuituma kwa maafisa wa serikali.
Kulingana na Dkt Mutua, wasafiri watakapofika Kenya watahitajika kutumia mtandao huo huo kuwasilisha kiwango chao cha joto mwilini kila siku kwa siku 14.
“Wale watakaokosa kufanya hivyo watatafutwa kwa anwani ambazo watapeana,” akasema.
Ingawa hayo yamenuiwa kufuatilia kama yeyote kati yao atakuwa ameambukizwa virusi vya corona katika kipindi hicho, haijajulikana jinsi serikali itafanikiwa kujua kama viwango vya joto ambavyo wageni watajaza vitakuwa ni vya kweli au kubahatisha.
Serikali ilikuwa imeamua wageni ambao hawaonyeshi dalili za kuugua Covid-19 wasilazimishwe kukaa karantini.