• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Serikali yajikaza kuwatuliza Watanzania

Serikali yajikaza kuwatuliza Watanzania

PETER MBURU na VALENTINE OBARA

SERIKALI Jumamosi ilijikakamua kurekebisha uhusiano wake na Tanzania baada ya ndege za Kenya Airways kupigwa marufuku kuingia katika nchi hiyo inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.

Uamuzi wa Tanzania kupiga marufuku ndege za Kenya ulitokana na kuwa serikali haikuijumuisha katika orodha ya mataifa ambayo yaliruhusiwa kuja nchini bila masharti makali.

Waziri wa Uchukuzi, James Macharia, alisema alijadiliana na mwenzake wa Tanzania na akamfafanulia kuhusu kanuni hizo za Kenya.

Kulingana naye, hakuna nchi iliyopigwa marufuku kuja Kenya, bali kanuni ni kwamba watu kutoka mataifa kadhaa ambayo hayakuwa kwenye orodha iliyotolewa watahitajika kukaa karantini wakija nchini.

“Kenya haijawahi kupiga marufuku ndege wala wasafiri kutoka Tanzania. Tulichofanya ni kutoa kanuni kuhusu safari kimataifa na tutakuwa tukifanya marekebisho mara kwa mara,” akasema.

Kenya Airways ilikuwa imepanga safari moja kuelekea Dar es Salaam jana ikirejelea usafiri wa kimataifa, lakini ikalazimika kuifutilia baada ya amri hiyo ya Tanzania.

Awali, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Bw Ababu Namwamba alikana kuwa kuna tofauti za kidiplomasia kati ya Kenya na Tanzania.

Bw Namwamba alisema uhusiano baina ya Nairobi na Dar es Salaam ni shwari, japo akidokeza kuwa ikiwa kuna tatizo lolote kuna mbinu za kulitatua.

“Hakuna tatizo lolote kati ya Kenya na Tanzania na uhusiano baina yetu ni shwari kabisa. Tunaendelea kushauriana kila wakati kuanzia ngazi za juu kabisa baina ya marais wetu na wizara za masuala ya nje,” akasema.

Hata hivyo, alishindwa kueleza ikiwa Kenya ilikuwa na habari kuwa Tanzania ingechukua hatua hiyo awali, licha ya kudai kuwa mashauriano yamekuwapo kila wakati.

“Hata kama kuna tatizo kuna njia za kutatua,” Bw Namwamba akasema.

You can share this post!

Wapinzani waenda mafichoni wakihofia kunaswa na serikali

Serikali yashauri familia zihakikishe maiti za wanaozirai...

adminleo