• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mutula Jr aongoza maseneta wa Ukambani kumkaidi Kalonzo

Mutula Jr aongoza maseneta wa Ukambani kumkaidi Kalonzo

Na BENSON MATHEKA

Maseneta wa kaunti tatu za Ukambani, wameapa kwamba hawatakubali kutishwa kuunga mfumo wa ugawaji wa pesa za kaunti utakaofanya kaunti zao kupoteza pesa wakisema mfumo wa sasa unafaa kudumishwa.

Wakizungumza Jumapili baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la African Brotherhood Church (ABC) mjini Machakos, maseneta Enoch Wambua wa Kitui, Boniface Kabaka (Machakos) na Mutula Kilonzo Jr (Makueni) walisema kwamba hawatakubali shinikizo zozote za kuwataka waunge mfumo huo.

Walisema kwamba ingawa kiongozi wa chama chao cha Wiper Kalonzo Musyoka ameunga mfumo unaolenga kugawa pesa za kaunti kwa kutegemea idadi ya watu, hawatauunga kamwe kwa kuwa utafanya kaunti Makueni na Kitui kupoteza pesa.

“Tumesukumwa na tunaendelea kusukumwa na vyama vyetu, tunasukumwa na watu kutoka kwingine. Hata wiki jana tulipopiga kura katika seneti tulikuwa tumesukumwa lakini msimamo wetu hautabadilika,” alisema Bw Mutula ambaye ni kiranja wa wachache katika seneti.

Bw Kabaka alisema ingawa kaunti yake ya Machakos itaongezewa pesa mfumo huo ukipitishwa, aliamua kuupinga kwa sababu utaumiza wakazi wa kaunti za Makueni na Kitui sawa na maeneo mengine masikini.

Seneta huyo ambaye ametofuatiana hadharani na Gavana wa kaunti yake Alfred Mutua kwa kupinga mswada huo alimtaka waziri wa fedha Ukur Yatani kusuluhisha mzozo kuhusu mfumo huo kabla ya kikao cha seneti leo.

“Bw Yattani angeita mkutano wiki jana. Tumeamua kusimama na Kenya na tunasisitiza kuwa tunataka mfumo unaotumika sasa udumishwe,” alisema.

Bw Wambua ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka alisema mikutano ya nje ya seneti ya kurai maseneta kuunga mfumo huo haitasaidia. “ Wanaweza kuita mikutano na wakutane. Hakuna anayewazuia kukutana lakini uamuzi wa pesa zitakavyogawiwa kaunti utafanyiwa kwenye kikao cha seneti Jumanne ,” alisema.

Bw Mutula alifafanua kuwa hakuna mipango ya kumuondoa spika wa seneti ofisini alivyonukuliwa akisema wiki jana.

Bw Musyoka aliunga mkono mfumo uliopendekezwa wa kutegemea idadi ya watu katika kila kaunti kugawa Sh316.5 bilioni zilizotengea kaunti kwenye bajeti ya 2020/2021.

Maseneta wamegawanyika kuhusu mfumo huo huku wengi ambao kaunti zao zitapata pesa zaidi wakiuunga mkono. Wale wanaotoka kaunti masikini wameukataa wakisema unabagua.

You can share this post!

Uvumbuzi wake unavyochangia kuimarisha taifa kiteknolojia

Ada za Idd ambazo ‘zimesahaulika’

adminleo