Serikali yashangaa bado mikusanyiko ya umma inafanyika
Na SAMMY WAWERU
Serikali haijaruhusu mikusanyiko yoyote ile ya umma kufanyika, ingali marufuku, amesema Dkt Rashid Aman, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya.
Waziri huyo amesema msimamo wa Wizara ya Afya haujabatilishwa na kwamba wanaoandaa mikusanyiko ya umma wanaenda kinyume na sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa Homa ya corona.
“Msimamo wa wizara ni; mkusanyiko wowote ule wa umma unakiuka sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti msambao wa Covid-19,” akasema Dkt Aman mnamo Jumatatu wakati akitoa taarifa ya hali ya virusi vya corona nchini, katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Alisisitiza msimamo wa Wizara ya Afya kufuatia swali la wanahabari kuhusu hafla za upashaji tohara zinazoendelea kufanyika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Wiki iliyopita, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa onyo kwa watakaotekeleza zoezi hilo la kitamaduni, akisema litaruhusiwa ikiwa mikakati maalum itawekwa.
Aidha, Bw Kagwe alidokeza kwamba serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wazee wa jamii ya eneo la Magharibi ili kupata mwelekeo.
Hata hivyo, kufuatia taarifa zilizofichuliwa na vyombo vya habari, imebainika zoezi hilo linafanyika wahusika wakionekana kutozingatia mikakati ya Wizara ya Afya kuzuia kuambukizwa corona.
Mnamo Jumatatu, Dkt Aman alisema serikali itafanya uchunguzi kubaini iwapo wanaoendesha upashaji tohara wamezingatia kanuni na mikakati iliyowekwa. “Mikakati tuliyoweka ni ya kutuzuia kuambukizwa corona. Anayekiuka sheria na mikakati hiyo, anakosea umma,” Waziri akasema.