HabariSiasa

Waabudu hela waeneza vifo nchini

August 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanapozama katika umaskini na kufa kwa maradhi na njaa, watu wenye ushawishi serikalini na wafanyabiashara walafi wameendelea kutumia majanga kujinufaisha na pesa zinazopaswa kuokoa maisha.

Ni watu wasiojali maisha ya binadamu na msukumo wao maishani ni kupata pesa kwa kutumia kila aina ya mbinu, na huwa wanacheka watu wanapokufa, kutembea uchi na kulala njaa.

Ni watu waliojawa na ushetani na tamaa ya pesa hivi kwamba wanawauzia Wakenya chakula chenye sumu mradi tu waweze kupata mabilioni ya kuwawezesha kuishi maisha ya anasa na kunyanyasa maskini.

Wakati huu wa janga la Covid-19, hawakuchelewa kumezea mate mabilioni yaliyotengwa kuwakinga Wakenya dhidi ya ugonjwa huo.

Serikali ilipotangaza ‘lockdown’ kukabiliana na virusi hivyo mnamo Aprili, wananchi wakiwa wamejifungia manyumbani hawa walikuwa wakiiba misaada ya kujikinga kutoka kwa wafadhili na kupora pesa za kukabili mkurupuko huo.

Wameshirikiana kuuza sanitaiza na vifaa feki vya kujikinga na virusi hivyo na matokeo yamekuwa ni maambukizi zaidi, mateso na vifo kuongezeka nchini.

Imefichuliwa kwamba walilenga kupora zaidi ya Sh223 bilioni ambazo serikali iliomba kutoka kwa wafadhili ili kukabiliana na corona.

Wengi wao wamehusishwa na ofisi zenye ushawishi mkubwa hapa Kenya.Baadhi yao walikuwa hata na ujasiri wa kuiba vifaa ambavyo serikali ilipatiwa na wafadhili akiwemo Jack Ma mara vilipowasili katika uwanja wa ndege wa JKIA, kisha wakaviuzia serikali kwa bei ghali.

“Hii haiwezi kufanyika bila kuhusika kwa watu wenye ushawishi mkubwa serikalini. Nyingi ya kampuni zinazofanya biashara na serikali ni za washirika wa wanasiasa na maafisa wakuu katika serikali. Mtu wa kawaida hawezi kuleta bidhaa nchini au kuingia uwanja wa ndege au bohari la shirika la serikali kuiba mali au kupata tenda ya serikali,” asema mtaalamu wa masuala ya biashara George Kibunja.

Kwa wahusika katika sakata hii, asema Bw Kibunja, janga la corona ni baraka kubwa kwao.Anasema licha ya wahudumu wa afya kutilia shaka ubora wa vifaa hivyo, kampuni zilizoviuza zililipwa zaidi ya Sh2 bilioni na zinaendelea kuvuna.

“Hivi ndivyo inavyofanyika wakati wa majanga yote ikiwemo ukame, ambapo wanasiasa na wafanyabiashara hushirikiana kuagiza chakula kutoka nje ya nchi, ambacho ubora wake ni wa kutiliwa shaka,” aeleza Bw Kibunja.

Mnamo 2018, serikali ilinasa maelfu ya magunia ya sukari iliyodai ilikuwa na sumu, japo ilikuwa imeidhinishwa na idara husika.

“Ni wazi kuwa wafanyabiashara wengi walio na ushawishi serikalini wamekuwa wakitumia njia za mkato kuingiza nchini bidhaa duni na hatari kwa maisha ya Wakenya. Hawajali hata kama watu watakufa. Maisha ya binadamu sio muhimu, kwao ni bora pesa,” asema Bw Kibunja.

Nchi inapokumbwa na ukame na mafuriko, Wakenya hufariki kutokana na njaa na kusombwa na maji licha ya serikali kutenga mabilioni ya pesa kusaidia waathiriwa.

Wachanganuzi wanasema ni kundi hili ambalo limekuwa likihakikisha Kenya haitekelezi sera na miradi ya kuongeza uzalishaji wa chakula, ili waendelee kuleta uhaba ambao huwapa fursa ya kuagiza chakula kutoka ng’ambo.

Badala ya kuwanunulia wakulima wa humu nchini mahindi waliyovuna, genge hili lilipora Sh1.9 bilioni zilizotengewa shughuli hiyo na wakawauzia mbolea feki ili wasipate mazao bora, na hivyo kuhakikisha kuna njaa kila mwaka.

Ni kundi hili ambalo pia liliiba pesa za ‘Kazi kwa Vijana’, ambazo zilinuiwa kuboresha maisha ya maelfu ya vijana nchini.

Mpango huo uliokuwa ukitekelezwa na Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) ulitumiwa kupora zaidi ya Sh1.2 bilioni.Matokeo yamekuwa ni vijana kuuawa na polisi baada ya kujiingiza katika uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya wanapokosa matumaini maishani.

Umaskini unapoongezeka, walio na ushawishi serikalini na washirika wao wa kibiashara husherehekea na huwa hawapepesi macho wakitumia pesa hizo haramu kununua majumba makubwa makubwa, magari ya kifahari na wengine ndege.

Ni kundi hili hili ambalo limevuruga sekta ya kilimo nchini na kuwaacha wakulima wa mahindi, chai, kahawa na miwa katika ufukara usio kifani, msongo wa mawazo, kushindwa kulisha na kuelimisha familia zao na kupoteza matumaini maishani.

Matokeo yamekuwa ni ongezeko la watu kujitia kitanzi wanapolemewa na maisha na ndoa kuvunjika.

Mabwenyenye hao pia wameporomosha viwanda kwa kuagiza bidhaa feki kutoka ng’ambo, hivyo kuvuruga uwezo wa kubuni nafasi zaidi za kazi.

Serikali nayo imechangia kushamiri kwa kundi hili la waabudu pesa kwa kukosa nia ya kuwakabili huku vita dhidi ya ufisadi vikigeuka wimbo wa kutuliza nyoyo za Wakenya, wakati walio na ushawishi na wakuu serikalini wakiendelea kuiba mali ya umma.