• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Visa vya corona sasa ni zaidi ya 25,000

Visa vya corona sasa ni zaidi ya 25,000

Na CHARLES WASONGA

VISA vya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ijumaa vilitimu 25,123 baada ya watu wengine 727 kuthibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Vile vile, watu 14 zaidi walifariki kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 413.

Wagonjwa hao wapya waligunduliwa baada ya sampuli 6, 814 kupimwa ndani ya saa 24.

Akiongea alipozuru kaunti ya Kisii kukagua kiwango cha utayari wa vituo vya afya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema 711 kati ya wagonjwa hao wapya ni Wakenya huku 16 wakiwa wageni.

Miongoni mwao, 539 ni wanauma huku 188 wakiwa wanawake, hali iliyopelekea Waziri Kagwe kuwataka wanaume kuwa kuzingatia masharti ya kudhibiti ugonjwa huo.

“Inaonekana kuwa sisi wanaume tunalemewa zaidi labda kutokana na hali kwamba wengi wetu kunakaidi masharti ya wizara ya afya. Nawaomba wanaume muwe waangalifu zaidi,” Bw Kagwe akasema.

Waziri pia alielezea kutamaushwa na ongezeko la visa vya maambukizi kaunti kaunti ya Nairobi ambayo Ijumaa iliandikisha vipya vipya 393 vya maambukizi.

Bw Kagwe aliwaomba wakazi wa Nairobi kutosafiri nje ya kaunti hiyo ila tu ikiwa ni lazima kwao kufanya hivyo.

Waziri alitangaza kuwa wagonjwa 674 walipona kutokana na Covid-19 nchini; 125 kati yao wakiwa wale ambao wamekuwa wakiuguzwa nyumban huku 549 ni wale waliokuwa wakitibiwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Kwa hivyo, kufikia Ijumaa jumla ya wagonjwa 11,118 walikuwa wamepona tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipogunduliwa nchini.

You can share this post!

Mbunge wa zamani Ramadhan Kajembe afariki

Nick Salat sasa yuko ‘ndaani’ ya serikali

adminleo