Nick Salat sasa yuko 'ndaani' ya serikali
Na CHARLES WASONGA
UKURUBA kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi unaendelea kuzaa matunda kufuatia uteuzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho cha jogoo Nick Salat katika wadhifa mkubwa serikalini.
Katika teuzi alizofanya hivi punde, Rais Kenyatta alimteua Bw Salat kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Ustawi wa Kilimo Nchini (ADC).
Kwenye tangazo lilichapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali, Rais Kenyatta alisema Bw Salat atahudumu katika wadhifa huo kwa mwaka mmoja.
“Kwa mujibu wa mamlaka yanayotokana na sehemu 7 (3) ya Sheria ya Mashirika ya Serikali, Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote Nchini, amteua Nicholas Kiptoo Arap Korir Salat kuwa mwenyekiti Bodi ya Shirika la Ustawi wa Kilimo hadi Juni 2021, kuanzia Agosti 7, 2020,” ikisema taarifa hiyo.
Alisema uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Baringo Benjamin Cheboi, ambaye alikuwa akishikilia wadhifa huo, umefutiliwa mbali.
Vile vile, kiongozi wa taifa alifutilia mbali uteuzi wa Bw Salat kama Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Nchini kuanzia Agosti 7, 2020.
Katika nafasi hiyo amemteua wakili Njoroge Nani Mungai ambaye atahudumu kuanzia Agosti 7, 2020 hadi Desemba 12, 2021.
Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, chama cha Kanu kilibuni muungano rasmi na chama cha Jubilee. Na wiki moja baadaye Rais Kenyatta alifanya mabadiliko katika uongozi wa Jubilee katika Seneti ambapo alimteua Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio kuwa kiongozi wa wengi.
Hii ni baada ya kumtimua mwandani wa Naibu Rais Williaam Ruto, Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kwa tuhuma za kuasi misimamo ya Jubilee.