Wizara yarudia kuhalalisha vyeti vya elimu
Na WANDERI KAMAU
WIZARA ya Elimu imeanza tena kuhalalisha vyeti vya masomo, baada ya kuvisimamisha tangu Machi kutokana na janga la corona.
Shule hizo zilisimamishwa punde tu shule zote zilipofungwa nchini, ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo. Kwenye taarifa jana, wizara iliwashauri wanaotafuta huduma hizo wawasilishe stakabadhi zao katika Jumba la Jogoo ‘B’, chumba nambari 600, jijini Nairobi, kabla ya saa sita na nusu mchana.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Ubora katika Wizara ya Elimu, Dkt Mary Gaturu, stakabadhi hizo zinapaswa kuwa zimewekwa kwenye bahasha na kufungwa vizuri.
“Wenyewe watakuwa wakizichukua siku inayofuata kati ya saa nane hadi saa kumi alasiri siku za Jumatatu na Ijumaa,” akasema. Maelezo ya mwenye stakabadhi yanapaswa kuandikwa nyuma ya kila bahasha.
Vile vile, wanaotafuta huduma lazima wawe na stakabadhi maalum za utambulisho kama paspoti ama vitambulisho vya kitaifa.
“Vyeti vya mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) ama Kidato cha Nne (KCSE) vitahalalishwa tu baada ya mmiliki kutoa cheti maalum kuonyesha amemaliza masomo katika shule alikosomea,” akasema.
Wanafunzi waliofanya mtihani wa KCSE kuanzia 2018 kurudi nyuma watahitajika vyeti vya mitihani yao badala ya nakala za matokeo yao.Kwa wale walio ughaibuni, itawalazimu kutoa nakala za paspoti zinazoonyesha tarehe walimotoka nchini na kufika kwenye mataifa walimo
.Zaidi ya hayo, alisema vyeti vya vyuo anuwai ama vyuo vya kiufundi lazima viwasilishwe pamoja na cheti cha kumaliza masomo na nakala za matokeo ya mitihani.
Kwa wale ambao wamewatuma watu kwa niaba yao, lazima wawe na stakabadhi zao maalum kama vitambulisho vya kitaifa. “Stakabadhi zote za watoto zinapaswa kuletwa na wazazi wao ambapo lazima wawe na vyeti halali vya tarehe ya kuzaliwa,” akaongeza.