Makala

AWINO: Wanasiasa wasitatize ufufuzi wa sekta ya sukari

August 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AG AWINO

IWAPO umewahi kuishi karibu na kampuni za kusaga miwa nchini, basi unaelewa maana ya ‘moshi mweupe’. Moshi huu huleta matumaini makubwa kwa wafanyikazi na wakazi kila unapoonekana.

Ni ishara ya hali ya ushwari kwa wafanyikazi na wafanyibiashara wanaotegemea kampuni hizi. Unapokosa moshi, hali ya huzuni hutanda kila mahali.

Tatizo sasa ni kwamba baada ya serikali kupitia kwa Halmashauri ya Kilimo na Chakula (AFA) kutangaza malengo yake ya kutafuta wawekezaji katika kampuni za sukari nchini kwa muda wa miaka 25, magavana wanaotoka katika enEo la ziwa Victoria, almaarufu Lake Victoria Economic Block (LVEB) tayari wamepinga zoezi hili eti kwa sababu wanataka kuhusishwa zaidi katika kutafuta suluhisho la kudumu.

Pendekezo lao, aidha, tayari limepingwa vikali na Chama cha Wakuzaji Miwa Nchini wakiongozwa na katibu Mkuu Richard Ogendo, akidai kwamba magavana hawana nia njema.Baadhi ya madai ya Bw Ogendo ni kwamba, kwa mfano, Kaunti ya Kakamega ambayo inaongozwa na Bw Wycliffe Oparanya ina kampuni mbili ambazo zinalipa wakulima kwa siku saba, ilhali za serikali huchukua zaidi ya miezi miwili kulipa.

Kaunti ya Busia pia ina kampuni mbili za kibinafsi za Busia Sugar na Olepito.

WAKULIMA KUUMIA

Hata hivyo, Kaunti ya Kisumu, licha ya kuwa na kampuni kama vile Kibos, Miwani, Chemelil na Muhoroni, haijashuhudia manufaa ambayo wananchi wameona.

Kwa mfano, Kibos inakabiliwa na tetesi za kutofuata kanuni kuhusu usafi wa mazingira ilhali nyingine zilizobaki hazileti faida.Kwa muda mrefu, serikali imekuwa ikitafuta mikakati ya kuimarisha maisha ya wakulima kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo ubinafshishaji.

Hata hivyo, baada ya siasa, hofu na vuta nikuvute baina ya wadau mbalimbali, serikali imeamua kutafuta suluhu kupitia hatua moja ambayo walikuwa wamejaribu hapo zamani.

Takriban miaka 30 iliyopita, kampuni za sukari nchini ziliwekwa mikononi mwa wawekezaji wa kibinafsi ambao walibadilisha maisha ya wakulima na wakazi wa maeneo ya ukuzaji miwa. Kwa mfano, wakati ambapo Wamarekani kwa jina Schaffer Group walikuwa wakiendesha shughuli katika kampuni ya Nzoia, wakulima walilipwa kwa wakati, mishahara ililipwa kwa wakati mbali na serikali na wafanyikazi kulipwa marupurupu kila mara. Hali ilikuwa vivyo hivyo wakati Mumias, Chemelil na Sony zilikuwa zikiendeshwa na wawekezaji wa Booker Tett.

Kampuni ya Muhoroni kwa wakati mmoja iliendeshwa na Mettah Group.Wakazi wa maeneo haya waliokuwa katika enzi za Mettah, Booker na Schaffer hawana lolote sasa isipokuwa kukumbuka enzi za kampuni hizi, ambapo maisha yalikuwa mazuri kwani walilipwa kwa wakati na miradi ya maendeleo ilikuwepo kwa wananchi majirani wa kampuni hizi. Pia hospitali na upanzi wa miti katika juhudi za kuimarisha mazingira iliimarishwa.

WAWEKEZAJI WA KIBINAFSI

Pengine hali hii ndiyo ilichochea serikali kutafuta wawekezaji kama ilivyokuwa zamani.Hasara na uharibifu ambao unazidi kushuhudiwa katika hali ya sasa ya kampuni hizi bado ni wazi kwani kampuni kama Chemelil imerekebisha mitambo yake mara tatu tu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, licha ya kwamba marekebisho yanafaa kufanywa kila mwaka.Kwa hivyo, kuendelea kupinga mbinu mpya ya kuendesha kampuni hizi ni kufifisha matumaini ya wakulima.

Magavana wa eneo la Ziwa Victoria wamethibitisha kwamba mwenye shibe kweli hajui mwenye njaa anahisi vipi, kwani huku wakulima wakizidi kudhoofika, wanaangalia tu jinsi ambavyo watajaza matumbo yao kwa kutetea malengo ya kibinafsi ya watu wachache wanaojaza mifuko yao.

Wakati umefika wa wakulima kutosikia sauti za viongozi wachache ambao si wakulima wa miwa wala watetezi wao wa kweli katika kilimo cha miwa.

Inafaa wasimame kidete na kuunga mkono juhudi za Waziri wa Kilimo Peter Munya katika kurudisha hiyo kama ilivyokuwa miaka 30 iliyopita kabla ya kuvamiwa na matapeli.

Bw Awino ni mwanamawasiliano na mwandishi kuhusu kilimo [email protected]