Habari Mseto

Wabunge wanne watetea Delmonte

August 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WABUNGE wanne wamewataka masoroveya wafanye juhudi ya haraka kupima upya ardhi ya kampuni ya Delmonte huku muda wa kukimiliki kipande chenyewe wa miaka 99 ukikaribia kukamilika mwaka wa 2022.

Wabunge hao wanaotoa ombi hili ni mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, Bw Simon King’ara (Ruiru), Joseph Nduati (Gatanga), na Jude Njomo (Kiambu).

Wabunge hao walisema kampuni hiyo inahitaji muda zaidi wa kuendesha shughuli zake katika ardhi hiyo ambapo ikicheleweshwa, hali hiyo itasababisha hasara kubwa kiuchumi.

Mbunge wa Thika Bw Wainaina alisema iwapo kampuni hiyo haitapewa muda zaidi wa kuendesha shughuli zake kwenye kipande hicho cha ardhi, bila shaka wafanyakazi zaidi ya 6,500 watapoteza ajira.

“Sisi kama wabunge tunashajiisha masoroveya wafanye haraka iwezekanavyo kupima kipande cha ardhi ukubwa wa ekari 22,000 ili kampuni hiyo ipate uhalisi wa eneo lake,” alisema Bw Wainaina.

Alisema ikiwa kuna ardhi iliyoko wazi ambayo kampuni itatwaa kwa umma, “bila shaka itanufaisha wananchi.”

“Ardhi ya aina hiyo itajengwa viwanda, shule, nyumba za kodi nafuu na hata hospitali ya wananchi,” alisema Bw Wainaina.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alisema ni vyema kurefusha muda wa kampuni hiyo ya Delmonte ili wapate nafasi ya kuwahifadhi wafanyakazi walioajiriwa katika kiwanda hicho.

Wabunge hao walizuru kampuni hiyo mnamo Ijumaa wiki jana ili kujionea jinsi inavyoendesha shughuli zake.

Bw King’ara alisema kampuni hiyo huwalipa wafanyakazi mishahara ya Sh2 bilioni kwa kila mwaka.

“Serikali haiwezi kubaki kuona kampuni hiyo ikifungwa kwa sababu mkataba wa kukalia ardhi hiyo unakamilika,” alisema Bw King’ara.

Aliwataka masoroveya wafike haraka na kuhakikisha ardhi hiyo imepimwa upya na haki kupatikana.

Mbunge wa Gatanga Bw Nduati alisema sehemu ya ardhi ya Delmonte iko Kaunti ya Murang’a na imekuwa na mikakati kabambe ya kunufaisha wakazi wa huko.

“Kampuni hiyo ina mpango wa kufungua kiwanda eneo la Murang’ a,” alisema Bw Nduati.

Alisema wanatetea kiwanda hicho kwa sababu kitatoa ajira kwa wakazi wa Murang’a.

Naye mbunge wa Kiambu Bw Jude Njomo alisema kampuni hiyo ikifunga shughuli zake hapa nchini, basi Kenya itapoteza fedha za kigeni takribani Sh10 bilioni.

Alisema kampuni hiyo ina kiwango cha ardhi ekari 22,000 jambo alilosema ni vyema kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.

Alisema uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na nchi za nje unastahili kulindwa kwa vyovyote vile.