• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu TZ yafana

Maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu TZ yafana

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, Tanzania

VYAMA vya kisiasa Jumatatu vilizidisha maandalizi ya uchaguzi mkuu, huku siku rasmi ya kuanza kampeni ikikaribia.

Kampeni za uchaguzi zimepangiwa kuanza rasmi Agosti 26 Tanzania, na Septemba 11, 2020, visiwani Zanzibar.

Lakini jana, viongozi wa vyama vya ACT-Wazalendo na Chadema walitia motisha wanachama wao walipoandaa mikutano.

Katika Bandari ya Malindi iliyo Unguja, maelfu ya wanachama wa ACT-Wazalendo waliweka foleni hadi Darajani kama ishara ya kuwakaribisha mgombeaji urais Bernard Membe na mgombea mwenzake Prof Omary Fakih Hamad.

Alipohutubia wafuasi, Hamad alisema chama hicho hakina haja na mapendeleo yoyote kutoka kwa maafisa wa usalama wala vyombo vya habari vya taifa.

“Inafaa serikali ikome kuharamisha mambo yanapofanywa na vyama vya upinzani wakati yanachukuliwa kuwa halali yakifanywa na CCM,” akasema.

Kumekuwa na malalamishi kwamba serikali imezuia vyombo vya habari Tanzania kupeperusha habari kuhusu vyama vya upinzani.

Mwaniaji urais kupitia kwa Chadema, Tundu Lissu naye alisema kuwa hana imani na tume ya uchaguzi.

Alipohojiwa na kituo kimoja cha redio cha nchini Kenya jana, Lissu alidai kuwa tume ya uchaguzi haina uhuru.

Mwaniaji huyo wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikiri kuwa itakuwa kibarua kwake kushinda uchaguzi utakapofanywa Oktoba 28, mwaka huu.

“Sina imani na Tume ya uchaguzi Tanzania. Japo tume si huru hatutaawachia tutapigana kwa kila namna,” akasema Lissu.

Wakili huyo machachari alirejea nchini Tanzania mwezi uliopita kutoka Ubelgiji ambapo amekuwa akitibiwa baada ya kumiminiwa zaidi ya risasi 20 na watu wasiojulikana jijini Dodoma mnamo Septemba 2017.

Mwezi uliopita, Lissu aliambia wafuasi wake jijini Dar es Salaam kuwa watashtuka iwapo atavua nguo kwani mwili wake umeharibiwa kwa risasi.

Wakati huo huo, Lissu alidai Jumatatu kuwa serikali imezuia vyombo vya habari kumhoji.

Alisema tangu aliporejea nchini humo hakuna kituo cha habari ambacho kimejitokeza kutaka kumhoji.

“Wanachama wetu wameuawa na wengine kuumizwa bila hata uchunguzi kufanyika, haki za binadamu Tanzania zimekandamizwa miaka mitano iliyopita. Viongozi wengi wa Afrika wanaongoza bila kufuata sheria,” akasema.

Vyama vya siasa saba kati ya vyama 13 tayari vimechukua fomu ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa Oktoba 2020.

Kwingineko, mashirika ya kijamii nchini Tanzania yameshutumu vikali sheria mpya inayoyataka mikataba ya ufadhili wa zaidi ya Ksh1 milioni (Tsh20 milioni) kutoka kwa wahisani ughaibuni kuidhinishwa na serikali.

Mashirika ya kijamii yanasema kuwa hazina kuu inajikokota kuidhinisha mikataba hiyo hivyo kuyafanya kukosa fedha kutoka kwa wadhamini.

Mashirika hayo yanasema kujikokota kwa serikali kuidhinisha mikataba hiyo huenda kukasababisha miradi yao kukwama.

Mkurugenzi wa shirika la Haki Elimu John Kalaghe aliambia The Citizen kuwa kucheleweshwa huko kunasababisha wahisani wa ughaibuni kutilia shaka utendakazi wa mashirika ya kijamii nchini Tanzania.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa huenda sheria hiyo kali inalenga kudhibiti fedha zinazoingizwa nchini Tanzania kutoka kwa wahisani ughaibuni kutokana na hofu kuwa zinaweza kutumiwa kufadhili kampeni za upinzani.

  • Tags

You can share this post!

Serikali Lebanon yajiuzulu kutokana na presha kutoka kwa...

TAHARIRI: Busara iongoze leo mjadala wa seneti

adminleo