• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Busara iongoze leo mjadala wa seneti

TAHARIRI: Busara iongoze leo mjadala wa seneti

Na MHARIRI

SENETI leo Jumanne inatarajiwa kujaribu kwa mara nyingine kupata mwafaka kuhusu mfumo mpya utakaotumiwa kugawa fedha kwa kaunti.

Wiki iliyopita, maseneta, kwa mara ya saba, walishindwa kuelewana kuhusu suala hilo tata.

Mgawanyiko uliopo unahusu mfumo unaozingatia zaidi idadi ya watu katika kila kaunti au ukubwa wa eneo la kaunti.

Kwa upande mmoja, kuna wanaoamini pesa nyingi zinahitajika katika maeneo ambapo kuna idadi kubwa ya watu.

Kwa upande mwingine, viongozi wa maeneo ya kaunti kubwa ambazo hazina watu wengi wanalalamika kwamba hizo ndizo kaunti ambazo zilisahaulika kwa miaka mingi tangu Kenya ipate uhuru.

Kwa mtazamo wao, kaunti hizo zinatakikana kutengewa pesa za kutosha ili wafikishe maendeleo yao angalau karibu na kaunti ambazo zilikuwa zikiendelezwa miaka hiyo yote.

Kilicho wazi ni kuwa, hakuna eneo ambalo linastahili kuchukuliwa kuwa muhimu kuliko eneo lingine lolote lile katika nchi hii.

Inahitajika maseneta watumie busara ya kutafuta njia ambayo itanufaisha kila mwananchi bila kujali eneo anakotoka.

Tunaelewa kuwa ugavi wa rasilimali ni mojawapo ya vigezo vikuu vya siasa kote ulimwenguni, na hivyo basi ni lazima siasa kuingizwa katika mijadala aina hiyo.

Hata hivyo, inafaa wahusika wote katika mjadala huu ambao wanategemewa kutoa uamuzi wa mwisho wazingatie haki zilizokabidhiwa wananchi katika katiba iliyopitishwa 2010 watakapofanya uamuzi wao.

Katiba hii changa ilinuia kuleta usawa kwa kila mwananchi kitaifa.

Ijapokuwa itakuwa safari ndefu kabla tufikie azimio hilo kikamilifu, haifai tuwe tunashuhudia hali ambapo baadhi ya viongozi wanajikakamua kutupigisha hatua nyuma kwa sababu zao za kibinafsi.

Ugatuzi umewezesha kaunti nyingi ambazo zilikuwa zimedhulumiwa katika enzi zilizopita kupata mwanga wa kuanza kujikuza. Haitakuwa haki kama juhudi hizi zitaanza kubomolewa kupitia kwa mambo yasiyokuwa na msingi.

Maendeleo maeneo hayo yatakuwa na uwezo wa kuvutia idadi kubwa ya watu katika siku za usoni na itakuwa aibu kama wakati huo ukifika, kaunti zitapatikana zingali hazina miundomsingi muhimu ya kutosheleza mahitaji ya raia.

You can share this post!

Maandalizi ya kampeni za uchaguzi mkuu TZ yafana

Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi ajiuzulu

adminleo