• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Idadi ya simba yapungua – IUCN

Idadi ya simba yapungua – IUCN

Na WINNIE ATIENO

HUENDA simba wakatoweka kabisa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa, Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori ulimwenguni (WAP) limeonya.

Akirejelea takwimu kutoka kwa Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Viumbehai na Turathi (IUCN) meneja wa kampeni ya WAP Edith Kabesiime alisema idadi ya simba barani Afrika imepungua kutoka 200,000 katika kipindi cha karne moja ambapo sasa idadi yao ni 20,000.

“Changamoto za simba ni zile zinazosababishwa na shughuli za binadamu, lakini pia sababu za kimazingira. Idadi ya simba imepungua kwa miongo kadhaa watu wakichukua nafasi ambazo zamani wakiishi simba,” akasema Kabesiime.

Naye Waziri wa Utalii na Wanyamapori nchini Najib Balala alikiri kuwa licha kwa kuongezeka kwa idadi ya simba nchini miaka miwili iliyopita, bado kuna changamoto.

Kenya ina takriban simba 2489. Bw Balala aliwaonya wawindaji haramu dhidi ya kuwatega wanyama hao na kuwauwa.

Akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa kuhifadhi simba na fisi, Bw Balala alisema kuna haja ya kuwalinda wanyama hao.

Takwimu kutoka wizara hiyo zinaonyesha kuwa idadi ya simba imeongezeka kutoka 1,970 mwaka wa 2018 hadi 2,489 mwaka huu wa 2020.

“Agosti 10 huwa tunasheherekea siku ya simba duniani. Tunataka kuongeza idadi ya simba wetu,” alisema Bw Balala.

Shirika la Ulinzi wa Wanyamapori Ulimwenguni pia limeonya kwamba mfalme huyo wa jangwani yuko hatarini na huenda akatoweka kabisa endapo juhudi za kumtunza na kumlinda hazitazingatiwa.

Simba wa Kiafrika wanakumbwa na tishio kubwa kutokana na shughuli za kibinadamu hususan katika mbuga za wanyamapori.

Changamoto zingine zinazowakumba wanyama hao ni pamoja na uwindaji haramu wa samba ili kuuza viungo vya simba na kutengeneza dawa.

Simba huwindwa kwa kudungwa kwa sumu na kusababisha kifo chake, wakati mwingine majangili wanaotekeleza uwindaji haramu huweka mtego wenye sumu na kuhatarisha maisha ya wanyama wengine porini.

Barani Afrika simba wanapatikana katika mataifa 26.

You can share this post!

Balala ahakikishia wawekezaji sekta ya utalii wizara...

Familia kupewa mafunzo namna ya kuzika wanaofariki kutokana...

adminleo