• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mjadala wa fedha waingizwa ukabila

Mjadala wa fedha waingizwa ukabila

Na CHARLES WASONGA

MJADALA kuhusu mfumo mpya wa ugavi wa fedha miongoni mwa kaunti 47 Jumanne ulitekwa na ukabila katika Seneti.

Maseneta wengi waliochangia mjadala huo walitoa matamshi yaliyoonyesha ubabe baina ya makabila tofauti ya nchi.

Seneta wa Tana River, Ali Wario Guyo na mwenzake wa Mandera, Mohammed Mahmud, walidai kuwa mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha unapendelea jamii ambazo zimewahi kushikilia uongozi wa taifa.

“Kaunti kama zile za maeneo ya Mlima Kenya zimepata maendeleo kwa sababu zimetoa marais wa Kenya mara tatu. Watu wa kaunti ya Kiambu ambao wametoa rais wa nchini hii mara mbili waache kaunti zingine kama Mandera na Wajir ziongezewe fedha ili ziweze kuinuka kimaendeleo,” akasema Mahmud.

Kauli hiyo ilimkasirisha Seneta Maalum Isaac Mwaura aliyesema mfumo wa kugawa pesa haupasi kuchukuliwa kama ambao unapendelea maeneo ya makabila ambayo yamewahi kushikilia uongozi wa taifa.

“Hii dhana kwamba Kiambu haina umaskini kwa sababu imewahi kutoa Rais mara mbili ni potovu. Nawaalika wenzangu waje Kiambu na watashangazwa na kiwango cha umaskini kilichoko huko,” akasema.

Walikuwa wakichangia hoja kuhusu pendekezo la Seneta wa Nairobi, Johnstone Sakaja kwamba mfumo ambapo hakuna kaunti itakayopoteza fedha zozote utumike.

Kauli ya Seneta Mwaura iliungwa mkono na Naibu Spika Margaret Kamar aliyesema ingawa kaunti yake ya Uasin Gishu inachukuliwa kama itakayoongezwa fedha zaidi chini ya mfumo uliopendekezwa na kamati ya fedha, wakazi wengi ni watu kutoka jamii zingine.

“Uasin Gishu ina jumla ya wati 1.163 milioni na ni asilimia 40 ya idadi hiyo wanaotoka jamii ya Wakalenjin. Asilimia 60 ni watu kutoka kaunti zingine. Kwa hivyo, pesa zitakazoendea Uasin Gishu hazitafaidi Wakalenjin pekee bali watu kutoka jamii zote za Kenya,” akasema.

Seneta wa Siaya, James Orengo pia alionya kwamba mwelekeo ambao mjadala huo ulikuwa unachukua ni hatari kwa umoja wa nchi.

You can share this post!

Yafichuka Ikulu ilihusika kusukuma Elachi ajiuzulu cheo...

Ruto apuuza mpango wa kusukuma Raila Ikulu

adminleo